
Picha na Ikulu.30/11/2016.
………………………..
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 30.11.2016
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Zanzibar
itaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na
Kenya na kuahidi kurejeshwa utamaduni wa safari za meli kati ya Zanzibar
na Mombasa kwa kutumia meli yake mpya ya MV Mapinduzi II.
Dk. Shein aliyasema hayo leo, huko Ikulu
mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi wa Kenya katika
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Chirau Ali Mwakwere.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein
alimueleza Balozi Mwakwere kuwa mbali ya ujirani wa mipaka kati ya
Zanzibar na Kenya pande mbili hizo pia, zina udugu wa asili ambao
ulikuza uhusiano wa kiuchumi na kiutamaduni, hivyo ipo haja ya
kuuendeleza.
Aidha, Dk. Shein amelipokea mikono miwili
ombi la Balozi huyo la kuimarisha ushirikiano katika usafiri wa baharini
kwa kuanzisha safari za meli kati ya Zanzibar na Mombasa, jambo ambalo
Rais alisema kuwa limo katika mipango ya kutekelezwa.
Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar imedhamiria kurejesha safari za meli zilizokuwepo hapo siku za
nyuma baina ya Mombasa na visiwa vya Zanzibar na si muda mrefu safari
hizo zitaanza huku akieleza kuwa safari za Tanga, Mtwara, Dar-es-Salaam
na hata Comoro nazo zitajumuishwa.
Mbali na hilo, Dk. Shein aliunga mkono
wazo la Balozi Mwakwere la kubadilishana uzoefu wa kitaalamu kati ya
wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Zanzibar na vyuo vikuu vya nchini Kenya na
kueleza kuwa hatua hiyo itazidi kuimarisha uhusiano na ushirikiano
uliopo kati ya pande mbili hizo sambamba na kuinua sekta ya elimu.
Dk. Shein alimueleza Balozi Mwakwere kuwa
kumekuwa na uhusiano wa kidugu na wa kihistoria kati ya Tanzania na
Kenya hatua ambaye imeipelekea kuwepo kwa Ubalozi Mdogo wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania huko mjini Mombasa.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa nchi mbili
hizo zimekuwa na historia ya kusaidiana pale nchi moja wapo inapopata
matatizo, hivyo ana imani kubwa utamaduni huo utaendelezwa kwa manufaa
ya pamoja.
Nae Balozi wa Kenya katika Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Chirau Ali Mwakwere alimueleza Dk. Shein kuwa
Kenya inajivunia uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake
na Zanzibar na kuahidi kuukuza na kuuendeleza.
Katika kuendeleza na kuukuza uhusiano na
ushirikiano huo, Balozi Mwakwere alitoa ombi maalum kwa Dk. Shein
kurejeshwa utamaduni uliokuwepo hapo siku za nyuma za kuwemo usafiri wa
baharini kati ya Zanzibar na Mombasa.
Aidha, Balozi Mwakwere alimueleza Dk.
Shein haja ya kuwepo kwa uhusiano na ushirikiano wa kubadilishana uzoefu
na utaalamu wa wanafunzi kati ya vyuo vikuu vya Zanzibar na vile vya
kenya ili vijana waweze kuutambua na kuukuza uhusiano uliopo.
Balozi Mwakwere alitumia fursa hiyo kutoa
pongezi kwa Dk. Shein kwa kuendelea kuiongoza Zanzibar kwa amani,
utulivu na maendeleo na kuahidi kuwa Kenya chini ya uongozi wa Rais
Uhuru Kenyata itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi zake
hizo.
Alisema kuwa kwa vile Kenya hasa maeneo
yake ya ukanda wa pwani tamaduni, silka na desturi zake zimeshabihiana
na Zanzibar ni vyema uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo
ukaimarishwa zaidi hasa katika sekta ya biashara na utalii.
Aidha, alisema kuwa Serikali ya Kenya
imechukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha maeneo ya ukanda wote wa
Pwani ya nchi hiyo unaendelea kutunza utamaduni, silka na desturi zao
za asili.
Sambamba na hayo, Balozi Mwakwere
alipongeza hatua za kuendelea kuyalinda na kuyatunza Mapinduzi ya
Januari 12, 1964 ambayo yaliondosha unyonge na kuleta utu na demokrasia
na kuifanya Zanzibar iweze kujisimamia mambo yake wenyewe.
Balozi Mwakwere alitoa pongezi kwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na watu wake kwa kuendelea kuilinda na
kuitunza lugha ya Kiswahili ambayo imekuwa lugha maarufu ndani na nje
ya Bara la Afrika na kusema kuwa wananchi wa Kenya wamekuwa
wakikizungumza na kukipenda Kiswahili cha Zanzibar ambacho ndicho cha
asili.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment