![]() |
Jovina Bujulu – MAELEZO.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake
Duniani, ni hatua muhimu kwa wanawake kujipambanua na kufanya tathmini
jinsi wanavyoshiriki katika ujenzi wa taifa kiuchumi, kijamii na
kisiasa.
Serikali imeweka mikakati na mipango mbalimbali yenye lengo la kumkomboa na kumuinua mwanamke kiuchumi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto, mama Sihaba Nkinga hivi
karibuni alipokuwa akizungumzia mipango na mikakati mbalimbali
iliyofanywa na Serikali katika kumkomboa na kumuinua mwanamke kiuchumi.
Pamoja na kuwa wanawake wengi
wameamka na wanajishughulisha katika masuala mbalimbali ya kiuchumi,
Serikali pia inahakikisha inawawezesha ili waweze kufikia malengo yao
katika masuala ya kujiinua kiuchumi na kuondokana na dhana ya utegemezi.
“Serikali ina mipango mbalimbali
katika kuhakikisha kuwa wanawake wamewezeshwa kiuchumi, ikiwa ni pamoja
na kuanzisha benki ya Wanawake ambayo moja ya majukumu yake ni
kuhakikisha wanawake wanapata mikopo kwa kuzingatia viwango wanavyoweza
kulipa” alisema mama Nkinga.
Aliitaja mikakati mingine kuwa ni
pamoja na kuwa na mfuko wa maendeleo ya wanawake ambapo wanawake
wanapewa mikopo yenye riba nafuu ambayo wanamudu kuilipa.
Aidha, Serikali kwa kushirikiana
na wadau mbalimbali wameweza kuwasaidia wanawake katika masuala ambayo
yamekuwa yakiwasumbua kwa muda mfefu kama vile umiliki wa ardhi. Kupitia
elimu hii kwa sasa wanawake wanaruhusiwa kumiliki ardhi kisheria na
kuondoa utata kuhusu suala hili.
Pamoja na mikakati hiyo, Serikali
imeenelea kushirikiana na wadau kuhakikisha kuwa vikwazo mbali mbali vya
mitaji na mikopo vinaondolewa ili kuhakikisha kuwa wanawake wengi
wanapata fursa ya kukopa na kulipa kwa muda hivyo kuwa huru kuendelea na
shughuli zao za kiuchumi.
“Idadi kubwa ya wakina mama wapo
kwenye ujasiriamali na viwanda vidogo vidogo hivyo Serikali imekuwa
ikitoa elimu kwao na kuwahimiza kukopa kwenye vyombo na taasisi za fedha
kwa sababu huko wanakopa kulingana na uwezo wao na hii itawasaidia
kufanikisha shughuli zao za ujasiriamali“ aliongeza mama Sihaba .
Aliwaasa wanawake kuachana na
sekta isiyo rasmi na badala yake wajikite katika sekta rasmi maana huko
kuna uzalishaji mkubwa ambao utawapatia soko la nje na aliwataka
kuboresha bidhaa zao ili wawe tayari katika ushindani mkubwa zaidi
wakati nchi yetu ikielekea katika uchumi wa viwanda.
Akizungumzia fursa na mlingano wa
ajira kati ya wanawake na wanaume alisema kuwa upande wa ajira wote
wanawake na wanaume wana nafasi sawa na kinachozingatiwa ni vigezo na
sifa za waombaji wa ajira.
Katibu Mkuu huyo aliendelea kusema
kwa sasa hakuna kazi za wanaume peke kwani upo uhalisia juu ya
ushiriki wa wanawake wengi katika kazi za uhandisi, ukandarasi na
udaktari.
Alitoa wito kwa wanawake, jamii na
watanzania kwa ujumla kuitumia siku hii kutoa hamasa kwa wanawake na
kuangalia nafasi yao katika jamii kipindi hiki ambapo Tanzania inaelekea
katika uchumi wa kati na viwanda.
Ili kufikia azma ya uchumi wa
viwanda, ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha anadumisha Umoja wa
nchi yetu na Utanzania wetu kwa kuwashirikisha wanawake, kwa kutoa elimu
na kuwapa nafasi ili watoe mchango wao ipasavyo katika kuinua uchumi wa
nchi.
Aidha, mama Nkinga alihimiza jamii
kusimamia watoto wa kike na kuhakikisha wanapewa haki inayostahili ili
nao wafike mahali waweze kutoa mchango wao kwa taifa.
Siku ya wanawake duniani
huadhimishwa kila ifikapo tarehe 8, Machi kwa shughuli mbalimbali kama
vile maandamano na hotuba, pia wanawake hutumia nafasi hiyo kutathmini
mafanikio ya shughuli zao za maendeleo, changamoto zilizopo na kuweka
mikakati ya utatuzi wa changamoto hizo. Kauli mbiu ya mwaka huu inasema
“Tanzania ya viwanda, wanawake ni msingi wa mabadiliko ya kiuchumi.”
|
March 9, 2017
MIKAKATI YA SERIKALI KATIKA KUMUINUA MWANAMKE KIUCHUMI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment