![]() |
Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya
limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo
mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana
na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na
uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na
kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu. Kufuatia mapambano
yanayoendelea nchi nzima dhidi ya watu wanaojihusisha na uuzaji na
utumiaji wa dawa za kulevya pamoja na uuzaji na utumiaji wa Pombe kali
zilizopigwa marufuku [viroba], Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanya
misako na Mafanikio yaliyopatikana katika Misako ni kama ifuatavyo:-
KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI.
![]()
Mnamo tarehe 09.03.2017 majira ya
saa 21:00 usiku Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na
Maafisa wa TANAPA lilifanya msako wa pamoja huko katika Kijiji na Kata
ya Lupatingatinga, Tarafa ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya
na kufanikiwa kuwakamata watu watatu wakiwa na nyara za serikali.
Watuhumiwa waliokamatwa ni 1.
HUSSEIN KHAMIS [33] 2. ISSA MLAWI [31] na 3. ZACHARIA MUSA [36] wote
wakazi wa Kijiji cha Matwiga. Watuhumiwa walikamatwa na nyara za
Serikali ambazo ni vipande 9 vya meno ya tembo na mikia 2 ya twiga.
Watuhumiwa ni majangili. Upelelezi unaendelea na mara baada ya
kukamilika watafikishwa mahakamani.
KUPATIKANA NA POMBE KALI ZILIZOPIGWA MARUFUKU [VIROBA].
![]()
Kufuatia msako mkali uliofanywa na
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Maafisa wa Mamlaka ya
Chakula na Dawa [TFDA] dhidi ya wafanyabiashara wa Pombe Kali
zilizopigwa marufuku nchini [viroba] limefanikiwa kuwakamata
wafanyabiashara wawili ambao ni ERASMO DANDA [50] Mfanyabiashara na
Mkazi wa Ihanga Wilaya ya Mbarali ambaye alikamatwa akiwa na pombe kali
zilizopigwa marufuku na serikali aina ya “viroba original” boksi 99
zenye thamani ya Tshs 9,768,000/= zikiwa zimehifadhiwa katika stoo
yake.
Mtuhumiwa mwingine aliyekamatwa ni
JOYCE BATHLOMEO [36] Mfanyabiashara na Mkazi wa Kibaoni Wilayani Chunya
akiwa na pombe kali zilizopigwa marufuku na serikali viroba vya aina
mbalimbali ambazo ni “high life” paketi 180 na aina ya Fiesta paketi
450 zikiwa zinauzwa katika duka lake la jumla.
Watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
KUPATIKANA NA VIPODOZI VILIVYOPIGWA MARUFUKU NA SERIKALI.
![]()
Mnamo tarehe 06.03.2017 majira ya
saa 13:00 mchana Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako kwa
kushirikiana na maafisa wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tawi la Mbeya
[TFDA] katika eneo la Rujewa lililopo Kata na Tarafa ya Rujewa, Wilaya
ya Mbarali na Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kumkamata mfanyabiashara mmoja
aliyefahamika kwa jina la ASUNGUKYENI MBILINYI [45] Mkazi wa Rujewa
akiwa na vipodozi vilivyopigwa marufuku na Serikali aina mbalimbali.
Vipodozi vilivyokamatwa katika
msako huo ni betasol lotion tube chupa 240, betasol cream chupa 144,
Epiederm cream tube 12, diproson cream tube 12, carlolight cream chupa
8, cocopup chupa 20 na citrolight chupa 6.
Jumla ya thamani ya bidhaa
yote iliyokamatwa ni Tshs. 1,380,000/=. Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani
mara baada ya upelelezi kukamilika.
WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya
Naibu Kamishina wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa
wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kuwafichua wahalifu na
mtandao wa wahalifu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ili
wakamatwe na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao. Aidha Kamanda
KIDAVASHARI anatoa wito kwa wananchi kufanya kazi na kuacha kujihusisha
na biashara haramu ya dawa za kulevya na uhalifu kwa ujumla kwani Jeshi
la Polisi halitavumilia aina yoyote ya uhalifu.
Imesainiwa na:
[DHAHIRI A. KIDAVASHARI – DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.
|
March 10, 2017
TAARIFA KUTOKA JESHI LA POLISI MKOANI MBEYA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment