Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Iddi Mgwatu (kushoto) akiteta jambo na Mkurugenzi wa Ukodishaji na Huduma za Vivuko TEMESA Mhandisi Japhet Maselle, nyuma yao ni Meneja wa TEMESA mkoani Mwanza Mhandisi Ferdnand Mishamo wakati wa majaribio ya boti Mpya ya MV Mkongo iliyojengwa kwa ajili ya kutumika katika eneo la Utete Rufiji Mkoani Pwani. Boti hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 40. |
Boti tatu kati ya nne mpya zilizokabidhiwa leo kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Kampuni ya Songoro Marine Boatyard baada ya kukamilika kwa ujenzi wake. Makabidhiano yamefanyikia jijini Mwanza na boti hizo zitasafirishwa kuelekea Pangani Tanga, Kilambo Mtwara na Msangamkuu Mtwara ili zianze kutoa huduma kwa wananchi. |
Boti Mpya ya MV Kuchele iliyokabidhiwa leo kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Kampuni ya Songoro Marine Boatyard baada ya kukamilika kwa ujenzi wake. Boti hii iliyojengwa kwa “fibre glass”ina uwezo wa kubeba abiria nane na itakuwa ikitumika nyakati za dharura katika eneo la Msangamkuu Mtwara. Makabidhiano hayo yamefanyika leo jijini Mwanza. |
Boti Mpya ya MV Tangazo iliyokabidhiwa leo kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Kampuni ya Songoro Marine Boatyard baada ya kukamilika kwa ujenzi wake. Boti hii iliyojengwa kwa “fibre glass”ina uwezo wa kubeba abiria 25 na itakuwa ikitumika nyakati za dharura katika eneo la Kilambo Mtwara. Makabidhiano hayo yamefanyika leo jijini Mwanza. |
Boti Mpya ya MV Bweni
iliyokabidhiwa kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Kampuni ya
Songoro Marine Boatyard baada ya kukamilika kwa ujenzi wake. Boti hii
iliyojengwa kwa “fibre glass”ina uwezo wa kubeba abiria nane na itakuwa
ikitumika nyakati za dharura katika eneo la Kilambo Mtwara. Makabidhiano
hayo yamefanyika leo jijini Mwanza.
Picha na Theresia Mwami – TEMESA Mwanza.
……………….
Na Theresia Mwami – TEMESA Mwanza
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi
na Umeme (TEMESA), Dkt. Mussa Iddi Mgwatu, leo amepokea boti nne
zilizokuwa zikijengwa na kampuni ya Songoro Marine Boatyard ya jijini
Mwanza. Dkt. Mgwatu amesema kukamilika kwa boti hizi ni utekelezaji wa
ahadi za Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Prof. Makame
Mbarawa alizozitoa kwa wananchi wa Pangani Tanga pamoja na Kilambo na
Msangamkuu Mtwara kwa nyakati tofauti.
Dkt. Mgwatu ameongeza kuwa boti
hizo nne zitatoa huduma za dharura hasa wakati wa usiku kwa ajili ya
kuhudumia wagonjwa na pia kutoa usafiri mbadala wakati vivuko vikubwa
vinapokuwa haviwezi kutoa huduma kutokana na changamoto mbalimbali
ikiwemo kupungua kwa kina cha maji katika maeneo ya Kilambo mkoani
Mtwara pamoja na Utete Mkoani Pwani.
Nae Mkurugenzi kutoka kampuni ya
Songoro Marine Boatyard Mhandisi Major Songoro amesema kuwa boti tatu
kati ya nne zilizokabidhidhiwa zimejengwa kwa kutumia “fibre Glass” na
boti moja imejengwa kwa kutumia chuma. Boti ya MV Kuchele ambayo
itapelekwa katika eneo la Msangamkuu Mtwara ina uwezo wa kubeba abiria
nane, sawa na boti ya MV Bweni itakayopelekwa katika eneo la Pangani
mkoani Tanga. MV Mkongo itakayopelekwa Utete mkoani Pwani ina uwezo wa
kubeba abiria 40 na MV. Tangazo itakayopelekwa Kilambo/Namoto Mtwara ina
uwezo wa kubeba abiria 25.
Aidha Dkt. Mgwatu ameishukuru
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano kwa kuwezesha ujenzi wa boti hizo na tayari
amemuagiza mkandarasi huyo kuhakikisha anazisafirisha boti hizo kwenye
maeneo husika haraka iwezekanavyo ili wanachi waanze kunufaika na huduma
mbadala itakayotolewa na boti hizo. Ujenzi wa boti hizo umefanywa kwa
kutumia fedha za ndani na umegharimu jumla ya shilingi milioni 415.
|
No comments:
Post a Comment