Na Thomas Nyindo.
Maofisa wa Idara za Sera na Mipango kutoka Wizara, Idara
na Wakala za Serikali wametakiwa kuongeza ufanisi na ubunifu katika kuandaa na
kusimamia miradi ya maendeleo ili kuharakisha malengo ya Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2025.
Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu
Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bw. Maduka Kessy wakati akifungua mafunzo
ya Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma yanayoendelea katika ukumbi wa
Chuo cha Mipango Dodoma.
Kessy alieleza kuwa mafunzo hayo
yanalenga kuwajengea uwezo maofisa wanaosimamia masuala ya Sera na Mipango
katika kuibua na kutekeleza miradi ya maendeleo, hususan, ile inayogharamiwa
kwa fedha za Serikali ili kufanya Tanzania kuingia kwenye nchi za kipato cha
kati kama ilivyoaninishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo.
“Mipango ya maendeleo tunayojiwekea,
kama taifa, inapaswa kutafsiriwa katika miradi na programu za utekelezaji,
hivyo mafunzo haya yatatusaidia kuongeza ufanisi, ubunifu na uwajibikaji katika
kuandaa miradi na kusimamia miradi yenye tija kwa wananchi,” alisema Kessy.
Aliwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo
kuwa wao ni miongoni mwa wadau muhimu katika kuifanya Tanzania ipige hatua za
maendeleo kwa kuwa ndio wanaohusika katika kupanga na kusimamia utekelezaji wa
miradi ya maendeleo.
Aidha, Kessy alieleza kuwa mafunzo hayo
yatawasaidia washiriki kuongeza ufanisi na ubunifu katika kuchagua miradi,
kutafuta fedha za ugharamiaji na kuboresha uratibu wa kufungamanisha
uwekezaji wa umma kwa kubainisha hatua za kufuata katika kujumuisha miradi ya
maendeleo katika bajeti za maendeleo.
“Mwongozo huu utawasaidia kufanya
maamuzi katika kuchagua miradi sahihi ya uwekezaji katika sekta ya umma na
kuhakikisha ufanisi katika utekelezaji wake. Sote tunafahamu kuwa azma yetu ya
maendeleo kitaifa ni kufikia uchumi wa kipato cha kati ifikapo 2025,” alisema.
Kaimu Katibu Mtendaji huyo alieleza
kuwa zipo changamoto zinazokabili usimamizi wa miradi ya maendeleo, kuanzia
hatua ya kubuni, kutekeleza hadi kukamilisha miradi hiyo. Kwa hiyo Mwongozo wa
Usimamizi wa Uwekezaji waRasilimali za Umma ni mojawapo ya maandiko muhimu
ambayo yamebuniwa kukabiliana na changamoto hizo.

No comments:
Post a Comment