Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
MBUNGE
wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, amekabidhi pikipiki kumi,
zilizogharimu sh. Mil. 22.5 kwa maafisa mifugo wa kata, ili waweze
kuwafikia wafugaji wote, kupeleka sera ya kufuga kisasa na kuondoa
migogoro na wakulima. Aidha amekemea tabia inayofanywa na baadhi ya
wafugaji ya kufuga kizamani kwa kuswaga makundi ya ng’ombe kwenye eneo
moja hali inayosababisha kuharibu rutuba.
Akikabidhi
pikipiki hizo, huko Lugoba Ridhiwani alieleza, vyombo hivyo vya usafiri
vikatumike kusimamia majukumu waliyonayo badala ya kuvitumia kwa
matumizi yao binafsi. Aliwataka jamii ya wafugaji kuachana na mtazamo
hasi wa kufuga kizamani mifugo lundo isiyo na tija pamoja na kuingia
katika maeneo ambayo hayajatengwa kwa ajili yao.
Ridhiwani,
alieleza kuwa wafugaji hasa wa kimasai wanaamini kuwa na ng’ombe wengi
ndio utajiri, waondoe dhana hiyo kwani sio sifa, wajaribu kufuga mifugo
michache na kujiwekea kasumba ya kufuga kwenye mazizi. Hata hivyo,
alimpongeza mkurugenzi wa halmashauri ya Chalinze, Edes Lukoa kwa
kusimamia na kuyafanyia kazi maazimio ya madiwani ambayo huwa wakitoa.
Ridhiwani,
alito mafuta lita tano kwa kila pikipiki na kuahidi kuangalia
uwezekano wa kufanya utaratibu kila mwezi kwenye posho zinazokwenda
katika kata maafisa mifugo hao wataongeza japo 5,000 kwa ajili ya mafuta
ya pikipiki hizo.
Kwa
upande wake mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Lukoa alisema pikipiki hizo
zimenunuliwa kutokana na mapato ya ndani ya halmashauri. Alizitaja kata
zilizokabidhiwa usafiri huo kuwa ni sanjali na Vigwaza, Kibindu,
Mbwewe, Talawanda, Msata, Kimange, Kiwangwa, Miono, Ubena Zomozi na
Mandela.
Mbunge
wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete akifurahi jambo na baadhi ya
watendandaji wakati wa zoezi la kukabidhi pikipiki hizo.
Lukoa
alieleza kwa msimu wa bajeti 2017/2018 wanatarajia kununua pikipiki
nyingine 15 kwa ajili ya watendaji na nyingine nane kwa ajili ya maafisa
mifugo wa kata na vijiji. Aliwashukuru madiwani kwa ushirikiano na CMT
kwa mchango wao mkubwa katika kutoa maazimio yaliyotakiwa yatekelezwe
na halmashauri na sasa yamefanikiwa. Lukoa alifafanua, kila afisa mifugo
wa kata anayekabidhiwa pikipiki atasaini mkataba wa makubaliano na
mwajiri wake na atatakiwa kuchangia asilimia 50 ambayo ni sawa na sh.bil
1.125 ya sh.bil 2.250 ambayo ni bei ya kukunuliwa atakayokabidhiwa kwa
kipindi cha miaka mitano.
“Hali
hiyo itasaidia kutunza pikipiki kwa kuwa itakuwa ni mali yao baada ya
kumaliza kuilipia malipo wanayokatwa yatawezesha kununua pikipiki
nyingine ili kuimarisha huduma za ugani’alisema Lukoa.
Nae
afisa mifugo na kilimo katika halmashauri ya Chalinze ,Bagamoyo Issack
Kama,alisema wapo maafisa mifugo wa kata na vijiji 26 ambao wanapaswa
kutoa huduma za ushauri wa kitaalamu kwa wafugaji waliopo kwenye vijiji
68 vilivyopo humo .
Alibainisha
kati ya maafisa hao wanne pekee ndiyo wana pikipiki na wengine 22
hawana hali iliyokuwa ikisababisha kushindwa kuwafikia wafugaji na
kuwapa huduma zinazostahili.
Kama
alisema ili wafugaji waweze kupata mafanikio katika ufugaji wanapaswa
kufuata kanuni bora za ufugaji kupitia ushauri wa maafisa mifugo wa kata
na vijiji.
Katika
hatua nyingine,baadhi ya maafisa mifugo waliokabidhiwa vyombo hivyo vya
usafiri akiwemo afisa mifugo kata ya Talawanda Enerst Lesi,wa kata ya
Mbwewe Rashid Mdemu walishukuru kupata pikipiki hizo kuwafikia wafugaji
na kuboresha huduma za ugani ukizingatia wafugaji wengi wanakaa mbali.
Mdemu
alielezea,kata ya Mbwewe ina vijiji sita hivyo ilikuwa ni vigumu
kuvifikia vyote hasa katika kutoa elimu mbalimbali na kufanikisha zoezi
la kupiga alama (chapa)mifugo ili iwe rahisi kutambulika. Akitoa
shukrani ya pamoja afisa mifugo kata ya Msata, Agripina Silau ,alisema
usafiri huo wameupokea katika muda muafaka .
Sehemu ya pikipiki hizo.
Alimhakikishia
mbunge huyo kuwa watakwenda kuwajibika kikamilifu ili kuleta mabadiliko
na kutatua changamoto ya migogoro ya wakulima na wafugaji licha ya
kwasasa kuonekana kuanza kupungua. Usajili wa mifugo na kuweka alama
kwenye mifugo usafiri huu umekuja muda muafaka.
Kwa
mujibu wa sense ya mifugo ya mwaka 2012,halmashauri ya Chalinze ina
jumla ya ng’ombe 240,000,mbuzi 94,000,kondoo 54,000,kuku 380,000 na
wanyama wengine.
No comments:
Post a Comment