Na Tiganya Vincent
RS –TABORA
20 August 2017
SERIKALI ya Mkoa wa Tabora
imeiagiza Kampuni ya Jossam & co Ltd kuhakikisha inakamilisha
barabara ilizopewa za Uledi na Mwenge katika Manispaa ya Tabora hadi
kufikia mwishoni mwa Mwezi Septemba mwaka huu.
Agizo hilo limetolewa jana na Mkuu
wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri baada ya kutembelea ujenzi wa
barabara hizo zinazojengwa katika Kata ya Uledi na Isevya ili kujionea
maendeleo na kuhakikisha kama mjezni amezingatia upana na urefu
ullioandikwa katika makubaliano ya mkataba.
Alisema kuwa kiasi cha shilingi
milioni 700 zilizopangwa na Manispaa ya Tabora kutumika kukamilisha
mradi huo ni fedha nyingi ni vema Mkandarasi anayejenga mradi huo
akahakikisha anajenga katika kiwango bora na kwa upana na urefu uliomo
katika mkataba ili thamani ya pesa ionekane.
Mkuu huyo wa Mkoa aliwaagiza
Watendaji wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kuhakikisha
wanasimamia kwa karibu ujenzi wa barabara hizo unazingatia matakwa
yaliyoelezwa katika Mkataba wa Ujenzi ili barabara hizo ziweze kutumika
kwa muda mrefu bila kuharibika.
Awali Mhandisi Msaidizi kutoka
Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Tabora Stephen
Warioba alisema kuwa ujenzi wa barabara hizo unahusisha njia za waenda
kwa miguu na ipaswa inamalize katika kipindi kilichoelezwa katika
Mkataba.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mwl.
Queen Mlozi alimwakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa atafuatilia kwa karibu ili
kuhakikisha kuwa kazi inayofanyika katika eneo husika inazingatia mambo
yote yaliyomo katika Mkataba na sio nje ya hapo.
Mkurugenzi Mtendaji wa
Manispaa ya Tabora Bosco Ndunguru alisema kuwa baada ya ujenzi wa Mradi
huu kukamilika kutakuwepo na zoezi la upandaji wa miti na maua kando
kando ya barabara.
No comments:
Post a Comment