Na Mwandishi Wetu
KAIMU Mkurugenzi Mkuu
wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela amewataka
viongozi wa wafanyakazi kupitia matawi mawili ya Chama cha Wafanyakazi, TAA Makao Makuu na
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), kutenda haki kwa
kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi wote bila kubagua na kuwasilisha kwa
mwajiri ili yaweze kufanyiwa kazi kwa wakati.
Bw. Mayongela ametoa
kauli hiyo jana wakati viongozi wa matawi hayo walipokwenda kujitambulisha
ofisi kwake TAA Makao Makuu, ambapo alisisitiza kuwa wafanyakazi wa chini ndio
wenye matatizo makubwa lakini wamekuwa hawasikilizwi na kutatuliwa matatizo yao
kwa wakati.
“Ninashukuru uongozi
mmekuja kuonana nami, ninahitaji ushirikiano wenu kama chama cha wafanyakazi,
muwatumikie wafanyakazi kwa kutenda haki mkisikiliza matatizo ya kila mmoja na
kufikisha sehemu husika na ninawaahidi kuwa nanyi bega kwa bega kutatua
matatizo ya wafanyakazi kwani wao ndio wanafanya TAA iwepo, endapo wakifanya
kazi bila manung’uniko wala makundi, mamlaka yetu itasonga mbele kwa kuwa
uongozi sio kupigana vita bali tunatakiwa kujenga na kuwa kitu kimoja.” amesema
Bw. Mayongela.
Hatahivyo amesema, kwa sasa
yupo mbioni kuangalia namna ya kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kupitia makusanyo yatakayotokana na
vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuongeza tija na ufanisi wa kazi, kwa kuwa
inaonekana wengi wamekata tamaa kutokana na kufanya kazi nyingi na wakati
mwingine kupitiliza muda wa kazi wa kawaida bila kupata stahiki yeyote.
“Kwa msaada wa Mungu
nina imani atanionyesha wapi fedha zilipo na jinsi ya kuzitumia ipasavyo kwa
masuala ya msingi, na ninakusudia hadi kufika Desemba mwaka huu niweze kuboresha
maslahi ya wafanyakazi. Watu wanafanya kazi sana lakini maslahi ni madogo,
unaona kabisa jinsi mtu anavyoitumikia taasisi kwa moyo, lakini sura inaonesha
jinsi alivyokata tamaa, ninaamini kwa kufanya hivi itaongeza tija na bidii ya
kazi.” amesema Bw. Mayongela.
Halikadhalika, Bw.
Mayongela amesema atahakikisha wafanyakazi wanapata vitendea kazi vya uhakika kulingana
na kazi zao, zikiwemo bajaji, pikipiki na magari kwa ajili ya doria na kwa shughuli
za uendeshaji ndani Viwanja vya Ndege.
Pia amewataka viongozi
hao kuwa karibu na wafanyakazi ili kuhakikisha wanawahamasisha wanafanya kazi
kwa bidii, uaminifu na uadilifu ili kuondoa mianya na tabia za upokeaji wa
rushwa, kwa kuwa TUGHE ni daraja kati ya mwajiri na wafanyakazi.
Naye Mwenyekiti wa
TUGHE tawi la TAA Makao Makuu, Bw. Nasib Elias mbali na kumshukuru Kaimu Mkurugenzi
Mkuu kwa kuwapa fursa ya kukutana naye, lakini amemuomba kuendelea kudumisha
mahusiano baina ya mwajiri na chama cha wafanyakazi (TUGHE), na pia kumuomba
aitake menejimenti yake kuwa na utaratibu wa kuweka milango wazi kwa wafanyakazi
kama yeye ili waweze kusikiliza na kutoa majibu sahihi kwa baadhi ya masuala ya
kiofisi yanayowasilishwa na wafanyakazi kwao na sio kila jambo liwasilishwe
kwake.
“Tunakuombea kwa Mungu
akutie nguvu kwa haya unayotaka kufanya likiwemo la kuboresha maslahi ya
wafanyakazi kwa kuwa litasaidia kuamsha morali ya kazi kwa wafanyakazi, lakini
hii sera yako ya kuwacha milango wazi tunaomba nayo itekelezwe katika ngazi ya menejimenti
yako kwani kuna mambo ambayo yanaweza kumalizwa na Wakurugenzi na Mameneja wenyewe
na sio lazima yafike kwako, “ amesema Bw. Elias.
Katika kuboresha
maslahi ya wafanyakazi ambacho kimeonekana ni kipaumbele cha Kaimu Mkurugenzi
mkuu kwa wafanyakazi, Bw. Elias amemuomba kuangalia namna bora ya kusimamia
maslahi hayo ikiwemo kuuasili mkataba wa hali bora (SBA) kama inavyotekelezwa
na taasisi nyingine za serikali.
No comments:
Post a Comment