Na Frank Mvungi-MAELEZO, Dodoma.
Serikali imetoa takribani Shilingi
Bilioni 21 kwa ajili ya kuboresha shule 85 za Kata hapa nchini ili ziwe
na Kidato cha Tano na Sita hali itakayoongeza ubora wa kiwango cha
elimu na kuimarishwa kwa miundombinu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais Mhe. Selemani Jafo wakati wa kipindi cha TUNATEKELEZA
kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) siku za Jumatatu
na Alhamisi.
Akifafanua Waziri Jafo amesema
kuwa dhamira ya Serikalini katika kuboresha sekta ya elimu ambapo kila
mwezi imekuwa ikitoa takribani Bilioni 23 zinazotumika kugharimia elimu
bure hali inayochochea kuongezeka kwa wanafunzi wanaojiunga katika shule
za msingi na Sekondari .
“Tumejenga madarasa mengi na vyoo
vingi ili kuendana na kasi ya udahili wa wanafunzi na pia tutahakikisha
kuwa kuna kuwa na uwiano katika mgawanyo wa walimu katika maeneo
mbalimbali hapa nchini.
Aliongeza kuwa Serikali katika
kuboresha huduma za Afya imeshapeleka fedha katika vituo 172 kote nchini
ili kuboresha huduma zinazotolewa na pia watumishi katika sekta hiyo
wataajiriwa kwa kuzingatia mahitaji kutokana na nafasi zilizoachwa wazi
baada ya zoezi la ukaguzi wa vyeti feki.
Aidha Waziri Jafo aliwataka
Viongozi wote katika Mikoa na Halmashauri kusimamia vizuri miradi yote
ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali katika maeneo yao ili thamani
halisi ya fedha zilizowekezwa ionekane.
“Nawasihi watanzania walipe kodi
kwa kuwa fedha zinazotokana na kodi ndizo zinazotumika kutekeleza miradi
ya maendeleo na ni matumaini yangu kuwa maelekezo niliyotoa kwa
wakurugenzi kuhusu ukusanyaji wa mapato yatazingatiwa na watasimamia
kazi hiyo vyema na kubuni vyanzo vipya vya mapato”Alisisitiza Jafo.
Aidha Waziri Jafo amewataka
watumishi wa Wizara hiyo kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwa kuwa hadi
sasa watumishi zaidi ya 300 wameshachukuliwa hatua mbalimbali za
kinidhamu kwa kushindwa kutimiza wajibu wao.
Kwa upande wa sekta ya Viwanda
amebainisha kuwa wamejipanga vyema kutekeleza dhana ya ujenzi wa uchumi
wa viwanda kwa kutenga maeneo maalum ya uwekezaji katika Halamashauri na
Mikoa.
No comments:
Post a Comment