Serikali
imesaini mikataba minne na kampuni nne za ujenzi wa barabara yenye
thamani ya zaidi ya sh. bilioni 702 kwa ujenzi wa kilomita 402.
Tukio
hilo la kusaini mikataba hiyo limeshuhudiwa na Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, Mwakilishi Mkazi wa
Benki ya Mandeleo ya Afrika (AfDB), MarieHellen Minja, wabunge ambao
miradi hiyo ya Barabara itapita majimboni mwao, Wakala wa Barabara
Tanzania (TANROADS) na wakandarasi walioshinda zabuni.
Akizungumzia
utiaji saini huo, Waziri Mbarawa amesema fedha hizo zitatumika katika
ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Tabora (Usesula)- Koga
hadi Mpanda yenye urefu wa kilomita 335 na kilomita 67 kutoka Mbinga
hadi Mbamba Bay mkoani Ruvuma.
Waziri
Mbarawa amesema ujenzi wa barabara hizo ni utekelezaji wa ilani ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), na ahadi za Rais John Pombe Magufuli wakati
wa kampeni.
Aidha,
Waziri Mbarawa ametumia nafasi hiyo kuwataka wakandarasi walioshinda
zabuni kujenga barabara zenye ubora na viwango kwa kuzingatia muda wa
ujenzi.
Profesa
Mbarawa ameongeza kuwa nia ya Serikali ni kuona ujenzi wa barabara hiyo
unakamilika kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
“Naomba
TANROADS msimamie ujenzi wa barabara yenye ubora kwani wakandarasi
wengi ni wajanja na ikitokea mtu ameharibu asipewe nafasi kabisa ya
ujenzi wa barabara hapa nchini,” amesema Waziri Mbarawa.
Kwa
upande wake Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale,
amesema kuwa wakandarasi waliopewa kazi wametokana na uchambuzi mkubwa
uliofanyika kati ya wakandarasi 129 waliojitokeza mwaka 2016 kuomba
zabuni za ujenzi wa barabara hizo.
Mhandisi
Mfugale amefafanua kuwa ili kurahisisha ujenzi wa barabara hizo
wamegawa kwa wakandarasi wanne ambapo barabara ya Usesula hadi Komanga
kilomita 108 itajengwa na Kampuni ya Jiangxi Geo-Engineering Group
Corporation Limited ya China kwa gharama ya zaidi ya Sh.Bilioni 158 na
itajengwa kwa miezi 36.
“Komanga
hadi Kasinde kilomita 108 itajengwa na Mkandarasi Kampuni ya China Wu
Yi Co. Limited kwa zaidi ya sh.billioni 140 na Kasinde hadi Mpanda
kilomita 105 Mkandarasi Kampuni ya China Railway Seventh Group Co.Ltd
kwa sh. Bilioni 133,” amesema Mhandisi Mfugale.
Mhandisi
Mfugale ameongeza kuwa barabara ya Mbinga hadi Mbamba Bay kilomita 67
inajengwa na Mkandarasi China Henan International Corporation Group
Co.Ltd (Chico) kwa sh. Bilioni 129.
Amesema TANROADS imejipanga kusimamia ujenzi huo kwa kufuata viwango vinavyohitajika vya ujenzi wa barabara nchini.
Mwakilishi
Mkazi wa AfDB, Bi. Minja amesema ofisi yake itaendelea kutoa mchango
kwa serikali katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali nchini pale
watakapo hitajika.
Bi. Minja amesema kuwa matarajio ya AfDB ni kuona Tanzania inapata maendeleo kwa haraka na njia rahisi ni kupitia miundombinu.
Waziri
wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe ambaye barabara ya
Tabora hadi Mpanda inapita jimboni kwake ambapo amesema kuwa ujenzi huo
utafungua fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Kwa
upande wake Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya, ambaye
pia ni Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, amesema barabara
hiyo itakuwa kiungo muhimu kati ya Tanzania, Msumbiji na Malawi.
Amesema
kuwa Nyasa ina vivutio vingi vya utalii hivyo ujio wa barabara hizo
utakuwa njia rahisi ya kuwafikisha watalii eneo hilo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment