Hatimaye
pande mbili za familia ya mtoto ambaye wazazi wake walikamatwa na dawa
za kulevya hivi karibuni nchini China, zimekubaliana alelewe na upande
wa bibi mzaa mama yake.
Familia
hizo zilikutana jana kwenye ofisi za Ustawi wa Jamii Makao Makuu jijini
Dar es Salaam na kufanya mazungumzo yaliyofikia mwafaka huo.
Wazazi
hao, Baraka Malali na Ashura Mussa, walikamatwa Januari 19 mwaka huu
kwenye uwanja wa ndege wa Baiyun, Guangzhou nchini China wakiwa wamemeza
pipi 129 za dawa za kulevya.
Mtoto
huyo alirejeshwa nchini Alhamisi iliyopita katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), majira ya saa 7:42 mchana akiwa
ameambatana na Ofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki.
Akizungumzia
uamuzi uliofikiwa kuhusiana na familia ambayo itamchukua mtoto huyo,
Kamishna wa Sheria wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya
(DCEA), Edwin Kakolaki, alisema familia hizo zilikubaliana mtoto alelewe
na upande wa bibi mzaa mama ingawa watashirikiana katika matunzo yake.
“Upande
wa mama yake mzazi ndiko atakakolelewa kwa sababu alishawahi kukaa huko
kwa muda kwa hiyo upande wa baba yake wameridhia mtoto aendelee kukaa
huko.
Lakini makubaliano ni kwamba mtoto ni wa familia zote mbili na wataendelea kumlea kwa pamoja,” alisema.
”Hayo ndiyo waliyokubaliana kwa pamoja hapakuwa na ubishani na sisi tulikuwa tunashuhudia makubaliano yao.”
Wazazi
hao baada ya kukamatwa Januari 19, mwaka huu, walipimwa na kubainika
kuwa wamemeza dawa za kulevya na kuwekwa katika chumba maalumu. Malali
alitoa pipi 47 na Ashura alitoa pipi 82.
Wakati
wazazi hao wakiwa mahabusu, serikali ya China iliwasiliana na Tanzania
na kufanya utaratibu wa kumrudisha mtoto nchini huku wazazi hao
wakisubiri hatima yao mahakamani.
Watu wanaopatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya nchini China huhukumiwa adhabu ya kunyongwa.
Kwa Tanzania hufungwa kifungo cha maisha kwa yeyote atakayekamatwa na ‘unga’ kuanzia gramu 20.
Kakolaki
alisema bado hawajajua mzigo wa dawa za kulevya walikozichukulia kwa
sababu safari yao ya kwenda China waliianzia Zanzibar.
“Walianzia
safari yao Zanzibar na baadaye walikwenda hadi Nairobi wakatoka hapo na
kuanza safari yao moja kwa moja hadi Guangzhou, China. Sasa kujua mzigo
walichukulia wapi bado hatujajua, lakini si kwamba walipita katika
uwanja wetu wa Dar es Salaam,” alisema Kakolaki.
No comments:
Post a Comment