Viongozi
wa madhehebu ya dini walikutana jijini Dar es Salaam jana pamoja na
wanasiasa kujadili "hofu iliyotawala" miogoni mwa wananchi
inayosababishwa na kutokea kwa matukio ya mauaji na watu kutekwa nchini.
Viongozi
hao pia walijadili uimara wa taasisi za madhehebu ya dini, uimara wa
mfumo wa serikali, pamoja na uimara wa taasisi za vyama vya siasa tangu
kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Katika
siku za karibuni, mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT),
Akwilina Maftah (22) alifariki kwa kupigwa risasi na polisi akiwa kwenye
daladala jijini Dar es Salaam Ijumaa iliyopita.
Rais
John Magufuli alisema katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii ya
Twitter Jumapili "Nimeviagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi na
kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha tukio hili."
Rais
Magufuli pia alielezea kusikitishwa sana na kifo cha Akwilina, na kutoa
pole kwa familia, ndugu, wanafunzi wa NIT na wote walioguswa na msiba
huo.
Aidha,
kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ambaye pia alikuwa katibu wa
Chadema kata ya Hananasif, Daniel John, alikutwa ameuawa na mwili wake
kutupwa katika ufukwe wa Coco jijini Dar es Salama pia wiki iliyopita
baada ya kutekwa mwanzoni mwa mwezi na watu wasiojulikana.
Akizungumza
katika kikao hicho, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT)
Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Benson Bagonza alisema hofu nchini
bado ipo baada ya kuwapo kwa matukio ya watu kupigwa risasi na kutekwa.
"Sijawahi
kuona risasi za moto zikirushwa kwa raia, watu wanapigwa risasi mchana
kweupe, sasa inatakiwa tufike mahali tuseme basi," alisema Askofu
Bagonza.
Alisema viongozi wa dini wataendelea kuonya matukio kama hayo pindi yatakapotokea bila ya kujali nani yupo madarakani.
Naye
Amiri Mkuu wa Baraza Kuu na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Mussa Yusuph
Kundecha alisema ni kweli hofu miongoni mwa wananchi ipo baada ya kuwapo
kwa matukio ambayo hawajawahi kuyaona miaka ya nyuma.
Alisema hofu hiyo inatokana na baadhi ya matamshi ya viongozi wanayoyatoa kwa wananchi na viongozi wa vyama vya siasa.
Akizufungua
kikao hicho, Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia (TCD), James Mbatia
alisema:"Tanzania bado kuna hofu, vipo viashiria ambavyo siyo vizuri.
"Kuna Watanzania wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi, akiwamo binti Akwilina. Wengine wamepotea, wengine wametekwa na kuuwawa.
"Bado
kuna manung'uniko, malalamiko miongoni mwa wananchi, mauaji yanatokea,
Watanzania wana hofu juu ya matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu."
Mbatia
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha NCCR-Mageuzi, alisema lengo kuu
la mkutano huo lilikuwa kujadili lengo la 16 katika 17 ya malengo ya
millennia, ambalo linahusu amani, haki na taasisi imara.
Mkurugenzi
wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema
Watanzania siyo kwamba wana hofu tu, bali hata hali ya kuishi haipo.
Mwenyekiti wa Chama cha UDP, John Cheyo alisema kongamano hilo limejikita katika kuwa na mazungumzo ya kujenga amani.
Alisema
Watanzania wanahitaji kuishi kwa amani na kwamba watu wanapoandamana,
kuuawa, kukaidi amri ya polisi maana yake hakuna amani nchini.
Mjumbe
wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (Nec), Kilumbe Ng'enda alisema
Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye amani kati ya nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki, na Nchi za Maziwa makuu.
"Kwenye
nchi hamuwezi kukaa kama mpo peponi, lazima mtatofautiana," alisema
Ng'enda, "(lakini) Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye amani."
Viongozi
wengine wa dini waliohudhuria ni Askofu Dk. Alinikisa Cheyo ambaye ni
mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristu nchini, Mkuu wa Kanisa la KKKT, Dk.
Fredrick Shoo, Askofu Moses Matonya, Askofu Stephen Munga na Askofu Ebem
Mshiu.
Pia Sheikh Hassan Kebeke ambaye ni mwenyekiti mwenza wa kamati ya viongozi wa amani Mwanza alikuwepo.
No comments:
Post a Comment