Hakimu
mkazi mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, John Mpitanjia
amesema dhamana ya Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP),
Abdul Nondo ipo wazi.
Nondo amefikishwa mahakamani hapo leo Jumatatu asubuhi Machi 26, 2018.
Mpitanjia
amesema dhamana ipo wazi na Nondo anatakiwa kudhaminiwa na watu wawili
ambao ni wakazi wa Iringa, mmoja awe mfanyakazi wa Serikali, na
wanatakiwa waweke bondi ya shilingi milioni 5 pamoja na kuwa na mali
isiyohamishika.
Kwa sasa wakili wa Nondo, Jebra Kambole anashughulikia dhamana ya mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Nondo
anatuhumiwa kwa makosa mawili. Kosa la kwanza ni kuchapisha taarifa za
uongo mtandaoni Machi 7, 2018 akiwa Ubungo na kusambaza kwa kutumia
mtandao wa WhatsApp kuwa yupo hatarini.
Shtaka
la pili ni kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa umma mjini Mafinga
alipokuwa akitoa taarifa katika kituo cha Polisi Mafinga kuwa alitekwa
na watu wasiojulikana jijini Dar es Salaam na kupelekwa Kiwanda cha
Pareto cha Mafinga.
Alifikishwa
mahakamani hapo saa tatu asubuhi akiwa kwenye gari la Polisi kisha
kupelekwa katika mahabusu ndogo mahakamani hapo na kuingizwa katika
chumba cha mahakama saa 3:45 asubuhi. Kesi imeahirishwa hadi Aprili 4,
2018.
Mara
ya kwanza Nondo alipofikishwa mahakamani kuliibuka mkanganyiko kwa
kisheria kuhusu dhamana baada ya upande wa mashtaka kuomba asipewe kwa
maelezo kuwa bado maisha yake yapo hatarini.



No comments:
Post a Comment