Waziri
wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba, ameagiza kuwasilishwa kwa Mkuu wa Jeshi
la Polisi nchini (IGP) orodha ya watu wote waliohusika katika sakata la
korosho za Tanzania zilizokutwa na kokoto nchini Vietnam ili wakamatwe
na kuhojiwa.
Hata
hivyo, amesema taarifa zinasema jambo hilo si la kwanza kufanyika
nchini. Dk. Tizeba alitoa agizo jana baada ya kuwasilishwa taarifa ya
uchunguzi korosho hizo iliyotolewa na kamati iliyoundwa kuchunguza suala
hilo.
Akizungumza
baada ya kupokea ripoti hiyo, Dk. Tizeba alimuagiza Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo, Mathew Mtigumwe, kuwasilisha orodha hiyo kwa IGP ili hatua
stahiki zichukuliwe dhidi yao.
“Waende
sasa wakahojiwe rasmi na vyombo vya dola, naomba hili lifanyike leo
(jana) ili wahojiwe kwamba wewe fulani ulikuwa mahali fulani wajibu wako
ulikuwa huu hukufanya hivyo, na kama wakibainika wana kesi ya kujibu
sheria ichukue mkondo wake,” aliagiza Tizeba.
Alisema
katika ripoti hiyo kuna majina ya watu waliohusika katika kusimamia
shughuli yote ya usafirishaji wa korosho kuanzia iliponunuliwa,
makampuni ya usafirishaji, waliofanya ubadilishaji kwenye shirika la
meli nchini (Nassaco).
“Majina
yao yamo na Ofisa wa Serikali wa Mamlaka ya Mapato (TRA) aliyetakiwa
aweke ‘seal’ kwenye hizo kontena kwa wakati baada ya kuwekwa kwenye
magunia ili kujiridhisha kwamba alichokishuhudia kinawekwa kwenye kasha
hakitabadilishwa na kuweka lakiri ya serikali kwamba humo ndani kuna
mzigo uko ndani ya udhibiti wa forodha, huyu naye anafahamika kwa jina,”
alisema.
Alisema
kwanini baada ya kufungwa makontena hayo yalibaki kwa siku tano hadi
sita yawezekana hakukuwa na meli ya kusafirisha, lakini yale ya kusafiri
yanakwenda yanapata nafasi kampuni ya kimataifa ya kuhudumia Shehena za
makontena Bandarini (TICTS) ambapo makontena ambayo yamefika huwa
yanatoka kupisha yanayosafirishwa.
“Tutajua
huyu naye ni nani ambaye pia yumo humu ambaye alitakiwa kuyatoa Nassaco
kuyapeleka Ticts na TPA (Mamlaka ya Bandari), tutataka tujue hayo mambo
nyie haikuwa kazi yenu kuchukua hatua, kazi yenu ilikuwa ni kukusanya
taarifa,” alisema Tizeba.
Alisema
ubalozi wa Vietnam ulifikisha serikalini malalamiko rasmi kuhusu mawe
yaliyopatikana kwenye viroba vya korosho nchini humo.
“Mimi
binafsi niliongea naye na akanionyesha kwa namna mbalimbali jinsi
wafanyabiashara wa Vietnam walivyokuwa wamepokea korosho
zilizochanganyika na vitu mbalimbali ikiwamo mawe,” alisema Tizeba.
Alieleza
kuwa taarifa ya Balozi ilionyesha korosho imenunuliwa mkoani Lindi,
lakini akitazama mawe yaliyokuwamo sio ya Nachingwea au Liwale
kunakopatikana mwambao wa pwani.
Alibainisha
pia jambo jingine ambalo limeendelea kujitokeza ni kuwapo kwa mchanga
kwenye magunia ya korosho na siku nne zilizopita imegundulika kontena
moja lilikuwa limechanganywa na mawe katika Bandari ya Dar es Salaam.
Dk.
Tizeba alisema mtu amenunua tani 20 za Korosho zinaondolewa tani 3 au
1.5 badala yake yanaingizwa mawe au mchanga na michikichi.
Alisema
atampatia ripoti hiyo Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Prof.
Makame Mbarawa, ili aweze kuona mambo yanayohusu wizara anayosimamia na
kama kuna uwezekano wa kuboresha ufanyike.
“Pia
taasisi zingine za serikali zinazohusika na masuala haya ambapo kuna
maghala yanayosimamiwa na Wizara ya viwanda na biashara nitampa hii
ripoti Charles Mwijage,” alisema.
Alisema
kwa upande wa serikali wanaendelea na jitihada kupitia Wizara ya Mambo
ya Nje na kwamba leo au kesho watakutana na wabunge kutoka Vietnam.
“Tutakutana
nao tuzungumze hili suala la korosho tuliweke vizuri, tumekutana na
Balozi ambaye kasema wabunge hao wapo nchini na wangependa na wao
kusikia.Tulikuwa tunasubiri ripoti yenu ilituwape picha kamili" Alisema
Kilichomo ndani ya Ripoti
Makamu
Mwenyekiti wa kamati hiyo, yenye wajumbe tisa Khasim Mbofu, alisema
makontena yaliyokutwa na kokoto hizo ni kutoka Tanzania na pia limekutwa
kontena bandarini lenye mchanga badala ya korosho likisafirishwa
kupelekwa nchini humo.
Alisema
kamati ilipata uhakika kuwa makontena hayo yalitokea Newala mkoani
Mtwara na viashiria vikubwa vinaonyesha zilitoka Tanzania.
“Uthibitisho
ni namba ya kontena ambazo zilikutwa kule zipo katika kumbukumbu ya
bandari ya Dar es Salaam na bandari ya Nassaco, pia walibaini si jambo
geni kutokea nchini na kwamba vyama vya ushirika vya msingi vya
Pangateni, Mnyawi na Nguvumoja na Mkiu navyo vimeshawahi kukutwa na
tatizo hilo,” alisema.
Alieleza
wakiwa bandarini walipata habari kuwa kuna kontena ambalo lilidhaniwa
kuwa lina korosho zinazopelekwa Vietnam limebainika kuwa lina maboksi ya
mchanga.
“Tumeenda
kuona kontena lilosadikika kuwa liliwekwa korosho zilizobanguliwa
kwenda nchini Vietnam badala yake yamejaa mchanga na hili lilibainika
katika scanner,” alisema.
Alisema
walibaini baada ya korosho zilizokutwa na kokoto kuhamishwa kutoka
katika malori na kwenda katika makontena ilichukua siku nne kufunga
lakiri.
“Eneo
jingine la viashiria vya mchezo huu ni kwamba ulichezwa nchini kwa kuwa
kontena hizi ilichukua siku 10 kutolewa bandari kavu ya Nassaco kwenda
TICTS,” alisema.
Kadhalika, alisema wamebaini kuna mianya kati ya ghala kuu na bandarini na hakuna ulinzi wa kudhibiti.
“Tumetembelea
mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Mtwara, Lindi, maghala na viwanda vya
kubangua korosho na kufanya mahojiano na watu mbalimbali ukiwamo ubalozi
wa Vietnam,” alisema.
Mapendekezo
Makamu
huyo alisema vyombo vya uchunguzi vifanye uchunguzi wa kina kuhusu
bandari ya Nassaco ambako ndiko korosho hizo zilitolewa katika malori na
kuwekwa katika makontena kubaini uhalisia wake.
Pamoja
na hayo, alishauri Serikali ifunge scanner yenye nguvu itakayoweza
kubaini kilichomo ndani ya magunia ikiwa ndani ya kontena na pia
walibaini kuwepo kwa uhaba wa vitendea kazi katika bandari kavu ya
Nassaco kutokana na kuwapo kwa malori mawili badala 12.
Alisema
kamati ilishauri kupitiwa upya kwa sheria ya korosho na kanuni zake
zipewe upya ili ziendane na biashara ya zao hilo na pia kufungwa kwa
mizani katika bandari kavu ya Nassaco.
“Pia
bandari ya Mtwara iboreshwe ili kuwa na uwezo wa kusafirisha korosho
inayozalishwa katika mikoa ya kusini, na Serikali ihakikishe Mkoa wa
Pwani unaingia katika mfumo wa stakabadhi ghalani kwa sababu katika hizo
korosho zilizokutwa Vietnam kuna gunia 10 pia mbazo zilikutwa na
chikichiki,” alisema.
Aliongeza: “Yaani michikichiki inalimwa Kigoma sasa inakuwaje unakuta katika korosho?” alihoji.
No comments:
Post a Comment