KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

September 13, 2018

SEKTA YA MIFUGO KUCHANGIA ASILIMIA 9 YA PATO LA TAIFA

Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatekeleza mpango mkakati wa kuendeleza sekta ya mifugo unaotarajiwa kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye pato la Taifa kutoka asilimia 6.9 hadi 9%.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Abdallah Ulega amesema bungeni jijini Dodoma kuwa, utekelezaji wa mkakati huo pia unatarajiwa kukuza sekta ya mifugo kutoka asilimia 2.8 hadi 5.2%.

Wakati anajibu swali la Mbunge wa Kibaha Mjini, Silyvester Koka, Ulega amesema, mkakati huo una lengo la kupunguza na kuboresha mazingira rafiki na endelevu katika uzalishaji mifugo yenye tija kwa kuzalisha mitamba milioni moja kwa mwaka.

Wabunge wameelezwa kuwa mitamba hiyo itapatikana kutoka makundi ya ng'ombe wa asili kwa kufanya uhimilishaji. Koka alitaka kufahamu Serikali ina mpango gani kuboresha bidhaa za nyama nchini pamoja na mazao mengine yatokanayo na mifugo.

Ulega amesema, mkakati wa kuendeleza sekta ya mifugo utaimarisha upatikanaji wa uhakika wa maji, malisho na vyakula bora vya mifugo, utahamasisha matumizi ya teknolojia za ufugaji wa kisasa, utaboresha afya, masoko, biashara na kuongeza thamani ya mazao ya mifugo.

Amesema, mkakati huo utaongeza uzalishaji mazao ya mifugo ikiwemo idadi ya ng'ombe wa maziwa kutoka 789,000 hadi milioni tatu, utaongeza uzalishaji maziwa kutoka lita bilioni 2.4 hadi lita bilioni 3.8 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa Ulega, mkakati huo pia utaongeza uzalishaji wa nyama kutoka tani 679,992 hadi tani 882,100, utaongeza uzalishaji ngozi za ng'ombe, mbuzi na kondoo kutoka futi za mraba milioni 89 hadi futi za mraba milioni 98.9 na utaongeza uzalishaji mayai kutoka mayai bilioni 3.2 hadi mayai bilioni 6.4.

"Pia, mkakati unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za ugani, kuongeza uzalishaji wa chanjo za mifugo zinazozalishwa hapa nchini, kuongeza usindikaji wa mazao ya mifugo, pamoja na kuongeza usambazaji wa teknolojia za ufugaji bora ili kufikia wafugaji wengi zaidi"amesema Ulega.

No comments:

Post a Comment