Dar es Salaam. Mamlaka ya Usafirishaji wa Majini na Nchi Kavu
(Sumatra) imeruhusu mabasi ya usafiri jijini Dar es Salaam, maarufu kama
daladala, kufanya safari ndefu kwenda mikoa ya kaskazini kutokana na
mahitaji makubwa ya huduma hiyo katika kipindi cha sikukuu za Krismasi
na Mwaka Mpya.
Mkurugenzi mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe alisema
jijini hapa jana kuwa wamelazimika kuruhusu daladala hizo kukidhi
mahitaji ya usafiri kwenda mikoa ya Arusha na Kilimanjaro katika kipindi
hiki.
Alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kuona wingi wa abiria wanaokwenda kwenye mikoa hiyo kulinganisha na mabasi yaliyopo.
Pia, alisema Sumatra ipo katika hatua za mwisho
kuongeza magari makubwa matano yanayofanya safari za mikoa mingine ili
kukabiliana na hali hiyo.
“Kwa kweli hatukupanga kabisa kutumia hizo
daladala na ndiyo maana zimeanza kuruhusiwa leo (jana) kuanzia saa 4:00
asubuhi na zinatoza nauli ile ile iliyopangwa,” alisema Ngewe.
Baadhi ya daladala zikiwamo zenye usajili wa
kufanya safari zake kati ya Mbagala Rangi Tatu na Makumbusho zilikuwa
zikikaguliwa na kupewa kibali na maofisa wa Sumatra kabla ya kuanza
kubeba abiria wa mikoa hiyo.
Kaimu katibu mkuu wa Chama cha Kutetea Abiria
Tanzania (Chakua), Gordwin Ntongeji alisema hali hiyo ya uwingi wa
abiria ilianza kujitokeza mwishoni mwa wiki iliyopita.
“Jumamosi na Jumapili abiria wa mikoa hiyo
walikuwa wengi na baadhi yao walikosa usafiri, ndio maana unawaona leo
hii (jana) abiria wanakimbilia katika hizo daladala ili kuwahi sikukuu
za Krismas na Mwaka mpya,” alisema Ntongeji.
Mmoja wa abiria hao, Julius Peter aliishukuru
Sumatra kwa uamuzi huo akisema kuwa amehangaika kwa siku ya tatu
kutafuta usafiri wa kwenda Arusha kwa kuwa kila basi alilojaribu kukata
tiketi, aliambiwa limejaa.CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment