Dar/mikoani. Matokeo ya uchaguzi wa marudio wa viongozi wa
serikali za mitaa uliofanyika juzi yameonyesha kuwa pamoja na CCM
kuendelea kuongoza, chama hicho tawala kimepoteza viti katika maeneo
kadhaa.
Kabla ya uchaguzi wa juzi, CCM ilinyakua zaidi ya
asilimia 70 ya viti vyote baada ya uchaguzi wa kwanza uliofanyika
Desemba 14, lakini vyama vya upinzani, vikiongozwa na Chadema
vilikusanya viti vingi kwenye maeneo ambayo havikuwahi kupata viongozi
wa mitaa, huku vikiongeza idadi kwenye maeneo ambayo vilikuwa na viti
vichache.
Sura hiyo imeendelea kujionyesha kwenye matokeo ya uchaguzi uliofanyika Jumapili iliyopita.
Habari kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma,
Tabora, Geita na Kilimanjaro pamoja na wilaya za Sengerema, Mkuranga na
Kilombero, zinaeleza kuwa CCM imepata mitaa na vijiji 258, CUF 39,
Chadema 85 na ACT mtaa mmoja. Kwa matokeo hayo pamoja na yale
yaliyotangazwa Desemba 17, mwaka huu na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi,
CCM sasa itakuwa imejipatia jumla ya mitaa na vijiji 9,666 wakati
upinzani kwa ujumla wao umegawana nafasi 3,336.
Kwa mujibu wa matokeo hayo ya awali, CCM ilipata vijiji na mitaa 9,406 na wapinzani kwa pamoja walikuwa wamegawana 3,211.
Uchaguzi wa marudio
Katika Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam,
uchaguzi huo ulirudiwa katika mitaa 15, ambako CCM imeshinda mitaa sita,
Chadema na CUF mitaa minne kila kimoja.
Kwa ujumla CCM imeshinda kwa asilimia 72 katika
nafasi ya mwenyekiti wa mtaa, Chadema asilimia 14 na CUF asilimia 11.
CCM imepata pigo katika uchaguzi uliofanyika katika mitaa mitano ya
Manispaa ya Moshi baada ya kuambulia kiti kimoja tu, huku vingine
vikichukuliwa na Chadema.
Hata hivyo, chama hicho kimeongoza katika uchaguzi
huo mkoani Kigoma kilikoshinda katika maeneo mengi. Mwenyekiti wa
Chadema Wilaya ya Kasulu, Rajabu Bujoro alisema vyama vinavyounda Ukawa
vilishindwa kuungana na hivyo kutoa mwanya kwa CCM kushinda.
Mkoani Tabora, hadi sasa CCM imechukua vijiji 31
kati ya 71 vilivyofanya uchaguzi huo wa marudio, CUF vijiji vitatu,
Chadema 10 na ACT kimoja. Katika uchaguzi wa vitongoji, CCM imechukua
vitongoji 147 kati ya 290, Chadema 30, CUF saba na ACT vitatu.
No comments:
Post a Comment