KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

December 22, 2014

DKT KIKWETE KUHUTUBIA TAIFA LEO, KUJIBU MASWALI YANAYOWACHANGANYA WANANCHI

 
 Dar es Salaam. Masikio ya Watanzania leo yameelekezwa kwa Rais Jakaya Kikwete watakapokuwa wakisikiliza hotuba yake kwa Taifa inayotarajiwa kujibu maswali yapatayo 10 ambayo yanatarajiwa kutegua kitendawili cha kashfa ya uchotaji wa Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Maswali hayo yanatokana na maazimio ya Bunge ambayo yalionekana kuvuta hisia za wananchi katika kona mbalimbali za nchi ambako walikuwa wanafuatilia moja kwa moja mjadala wa Bunge hadi kupitishwa maazimio hayo.
Hotuba hiyo inayotarajiwa kutolewa wakati Rais atakapozungumza na wazee wa Dar es Salaam, ikiwa ni siku nne baada ya Kampuni za IPTL na Pan Africa Power Solutions (PAP) kukimbilia mahakamani kuzuia utekelezwaji wa maazimio ya Bunge.
Baadhi ya wasomi nchini wamesema hatua ya kuzuia utekelezaji wa maazimio hayo pamoja na kauli ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka kuwa akijiuzulu Rais atamshangaa, ni mambo yanayofanya hotuba ya Rais kusubiriwa kwa hamu.
Swali la kwanza ambalo wananchi wanasubiri jibu lake ni iwapo Rais Kikwete atatuliza kiu yao kuhusu kashfa hiyo ambayo imekuwa gumzo nchi nzima na hivyo kulegeza msimamo wa wahisani wa kuinyima nchi misaada.
Pili, wananchi wanasubiri kusikia iwapo Rais Kikwete ataagiza uchunguzi zaidi wa Takukuru, Polisi na vyombo vingine kama ambavyo azimio la kwanza la Bunge linavyotaka wahusika wachukuliwe hatua za kisheria kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Tatu, wanasubiri kwa hamu kuona hatua ambayo Rais Kikwete atachukua dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi pamoja na Profesa Tibaijuka kutokana na kutajwa katika maazimio hayo ya Bunge.
Kwa nyakati tofauti, viongozi hao wamekaririwa wakisema kuwa hawahusiki na kashfa hiyo. Mbali ya Profesa Tibaijuka kujitokeza kujitetea mwenyewe, baadhi ya wananchi wamejitokeza kuwatetea na kuwasafisha viongozi hao katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Nne, Je, atatengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Umeme (Tanesco) ambayo pia ilitakiwa kuwajibishwa ikiwa chini ya Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali Robert Mboma.
Tano, ili kuwachukulia hatua majaji waliotajwa, Aloysius Mujulizi na Profesa Eudes Ruhangisa, Rais Kikwete anatakiwa aunde Tume ya Kijaji ya kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili zinazowakabili, kinachosubiriwa kwa hamu ni kuona endapo ataunda tume hiyo.
Swali la sita linalohitaji jibu linahusu kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi. Kinachosubiriwa ni jibu la Rais Kikwete iwapo Serikali itaandaa na kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria iliyoiunda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia masuala hayo.
Vilevile, wananchi wanatazamia kupata suluhisho la gharama kubwa za umeme katika jibu la Rais Kikwete iwapo Serikali iko tayari kuinunua mitambo ya Kampuni ya IPTL kama ilivyopendekezwa na Bunge kwa lengo la kuokoa fedha za Tanesco zinazotumika kununua umeme kwa bei ya juu.CHANZO MWANANCHI

No comments:

Post a Comment