Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dk Alex Malasusa akimbariki mtoto baada ya kumalizika kwa ibaada ya Krismasi iliyofanyika katika Usharika wa Azania Front, Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis. |
Dar/mikoani. Kashfa ya uchotaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow inayoendelea kulitingisha Taifa, jana ilitawala mahubiri ya Sikukuu ya Krismasi katika makanisa mbalimbali nchini, viongozi wa dini wakionyesha kutoridhishwa na maelezo na hatua zinazochukuliwa.
Wakihutubia waumini wao, viongozi hao walitumia siku hiyo kukemea vitendo vya ufisadi, wizi na uzembe.
Hofu ya Escrow
Ujumbe wa Askofu wa Dayosisi ya Central Tanganyika
(DCT) wa Kanisa la Anglikana, Dk Dickson Chilongani ulilenga kueleza
hofu ya wananchi kutokana na sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, ugumu
wa maisha, ukosefu wa ajira, kukosa uhakika wa huduma bora za matibabu
na elimu pamoja na wimbi la viongozi waandamizi wasiokuwa waaminifu na
waadilifu.
Akihubiri katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu
mjini Dodoma, Askofu Chilongani alisema mbali na maisha ya ufukara na
ukosefu wa huduma, sakata la Escrow na hotuba ya Rais Jakaya Kikwete
aliyoitoa Jumatatu vimezidi kuzidisha hofu kwa Watanzania na kuwafanya
waonekane kama hawana tumaini.
Akitumia mtindo wa kuhoji, Askofu Chilongani
alianza kwa kuhoji, “Kitu gani kinakutia hofu unaposherekea sikukuu hii,
watu wengi tunaishi katika ulimwengu wa hofu kutokana na ufukara,
ukosefu wa huduma, tunajiuliza tutawasomeshaje watoto wetu, tutapataje
huduma bora za matibabu, yaani kila mmoja wetu ana hofu,” alisema.
Askofu Dk Chilongani alisema ingawa kila mtu ana
hofu yake lakini sakata la akaunti ya Escrow limejenga hofu kwa
mwananchi, kila mmoja akihoji na kutengeneza majibu yake jambo linalotoa
picha kuwa jibu sahihi halijatolewa au kupatikana.
“Mimi siyo mwanasiasa wala mtaalamu wa masuala ya
siasa lakini kuna hili sakata la Escrow ambalo juzijuzi Rais amelitolea
ufafanuzi, hili nalo linazidi kuwajengea wananchi hofu, wengine
wanakosoa maazimio ya Bunge, wengine wanataka Serikali itoe maamuzi
yenye tija kwa umma, yaani ni hofu tu,” alisema.
Escrow ni fedha za umma
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi, Anthony Lusekelo
alisisitizia kuwa fedha zilizochotwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow ni
mali ya umma kutokana na taarifa iliyowasilishwa na PAC bungeni.
Kauli hiyo inakuja baada ya Rais Kikwete kusema
fedha hizo ni mali Kampuni ya IPTL na zilikuwa Sh202 bilioni na si Sh306
bilioni kama inavyodaiwa.
Akihubiri katika kanisa hilo jana, Lusekelo
maarufu kama ‘Mzee wa Upako’ alisema: “Niliisikiliza kwa makini mwanzo
hadi mwisho (hotuba ya Rais) leo nimeona niseme machache kwamba fedha
hizo ni mali ya umma. Mimi siungani na hao wanaodai fedha hizi siyo za
umma lakini kwa hali hii hakuna jinsi inabidi tumwachie Mungu maana yeye
ndiye atakayeweza kutuvusha kutoka hapa tulipo,” alisema.
Padri: Viongozi wa dini waliotajwa wajipime
Paroko wa Parokia ya Mugumu, Serengeti, Padri
Aloisi Magabe amesema viongozi wa dini ambao wametajwa kuhusika na fedha
kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow wanatakiwa kujipima kwa kuwa
maadhimisho ya Krismasi yana maana kubwa, hivyo kuwa sehemu ya watu
wanaotuhumiwa si jambo jema.
Akihutubia katika ibada ya Krismasi, Padri Magabe alisema vitendo hivyo vinazidi kushika kasi lakini hatua hazichukuliwi.
Alisema ufisadi ulijichomoza kwa nguvu kwenye
Richmond, Epa na sasa Escrow, huku viongozi wa dini wakihusika, hatua
ambayo ni hatari huku akisema juhudi za kuwashughulikia wahusika
huchukua muda mrefu, chanzo kikiwa ni kulindana na rushwa. “Sina hofu ya
kusema waziwazi matukio kama hayo, nimefuatilia magazeti jinsi
wanavyojitetea, bado kuna haja ya kuwa wazi zaidi, maana nchi yetu ni ya
haki na usawa, tutaupataje usawa kwa ‘skendo’ kama hizi?”
Askofu Mkude: Nina imani kubwa na JK
Askofu wa Jimbo la Morogoro, Telesphol Mkude
amesema ana imani kubwa na Rais Kikwete kwa namna anavyolishughulikia
suala la kuwajibisha waliotajwa katika sakata la Tegeta Escow na
kuwaomba Watanzania kumpa muda wa kutosha ili aweze kuendelea kutoa
uamuzi ulio sahihi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa
katika ofisi ndogo ya Kanisa Kuu la Mt Patrick, Mkude alisema suala la
Escrow limepita katika mchakato mrefu na baadhi ya wameanza kuchukuliwa
hatua, wakiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema
aliyejiuzulu na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo Makazi, Profesa
Anna Tibaijuka aliyefukuzwa.
“Haya mambo yanaenda na uchunguzi, sidhani kama
Rais anaweza kutoa uamuzi pasipo kujiridhisha, pamoja na kuwapo kamati
iliyojiridhisha na uchunguzi na kubaini uchotaji wa fedha za umma,
lakini na yeye kwa nafasi yake anapaswa kujiridhisha kupitia jopo lake,”
alisema Askofu Mkude.
Hofu ya Mungu na ufisadi
Hofu ya Mungu imeelezwa kuwa ndiyo pekee
itakayoondoa wizi na ufisadi miongoni mwa viongozi na watendaji badala
ya kutegemea sheria pekee.
Hayo yalisemwa jana na Askofu Mkuu wa Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa wakati akihubiri
katika ibada ya Krismasi katika Kanisa la Azania Front, jijini Dar es
Salaam.
Kauli hiyo inafanana na ile iliyotolewa na
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Gloryland International la jijini Tanga,
Manase Maganga.CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment