Doha, Qatar. Serikali ya Qatar imesema iko tayari kuajiri
Watanzania katika nyanja mbalimbali za kitaalamu kwa kuwa taifa hilo
lina uhaba wa wataalamu katika maeneo mengi.
Hayo yako katika mazungumzo yaliyofanyika jana
kati ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh
Abdullah Nasser Al Thani ofisini kwake mjini Doha, Qatar.
Waziri Mkuu Pinda yuko katika ziara ya
kuzitembelea nchi za Falme za Kiarabu. Aliwasili juzi usiku na kupokewa
kifalme na mwenyeji wake huyo.
Akizungumza baada ya mkutano, Pinda alisema
Serikali ya Qatar imesema iko tayari kuwapa Watanzania ajira katika
maeneo mbalimbali.
“Kimsingi, waziri mkuu amekubali Watanzania kuja
kufanya kazi Qatar kwa kuwa hapa wengi ni wageni, tusubiri baada ya
mkataba tutakaotiliana saini wa kuwaleta Watanzania hapa,” alisema.
Alisema kuna baadhi ya Watanzania tayari
wameshaingia kwenye soko la ajira Qatar, lakini idadi haitoshi kutokana
na ukweli kuwa Qatar kuna kazi nyingi.
“Pia tutawekeana utaratibu wa kubadilishana wataalamu ili pande zote mbili zifaidike,” alisema Pinda.
“Waziri Mkuu ameniambia wao wana gesi lita za
ujazo trilioni 900, sisi Tanzania ni trilioni 53, sasa nimeomba
tushirikiane hapa kwa kuwa wao tayari ni wazoefu,” alisema.
Alisema kuwa Qatar ambayo ni ya 11 kwa utajiri
duniani, pamoja na kwamba ni nchi ndogo yenye idadi ya watu milioni 2.2,
wana uwezo mkubwa eneo la mafuta na gesi.
Pinda jana alitarajia kuwa na mazungumzo na Naibu
Waziri wa Nishati, Waziri wa Masuala ya Uchumi, Waziri wa Vitegauchumi,
Waziri wa Miundombinu na Usafirishaji na Waziri wa Kazi na Maendeleo ya
Jamii.
Baadaye usiku, alitarajiwa kukutana na Watanzania
wanaoishi na kufanya kazi Qatar na kisha kutembelea Bandari ya Qatar na
kufanya mazungumzo na maofisa wa bandari hiyo.
No comments:
Post a Comment