Katibu wa Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Operesheni Tokomeza, Bw.Frederick Manyanda.
Na. Mwandishi Wetu
Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Operesheni Tokomeza itakusanya taarifa
na kupokea malalamiko yaliyotokana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza
Ujangili Nchini mikoa ya Mikoa ya Arusha, Manyara, Tabora, Singida na
Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa tarehe 24 Desemba, 2014 na Katibu
wa Tume hiyo, Bw.Frederick Manyanda, Tume inatarajiwa kuendelea na zoezi
la kukusanya maoni na taarifa kuanzia tarehe 5 Januari , 2015 mpaka
tarehe 21 Januari,2015 katika maeneo mbalimbali ya kanda ya Kaskazini na
Kati Nchini.
Katika kutekeleza jukumu hilo, Bw. Manyanda ameeleza kuwa, Tume
itatembelea Mkoa wa Tabora tarehe 4 Januari 2015 mpaka tarehe 8 Januari
2015 na itakuwa Mkoa wa Singida tarehe 9 Januari,2015 mpaka tarehe 10
Januari,2015.
Aidha Tume itatembelea Mkoa wa Dodoma tarehe 11 Januari, 2015 mpaka
tarehe 12 Januari 2015. Vilevile, Wakili Manyanda ameeleza kuwa Tume
itakusanya maoni Mkoa wa Manyara kuanzia tarehe 13 Januari, 2015 mpaka
tarehe 16 Januari, 2015 na Tume itakuwa Mkoa wa Arusha tarehe 16 Januari
2015 mpaka tarehe 19 Januari,2015.
Mpaka sasa Tume ya Rais ya Operesheni Tokomeza imefanikiwa kukusanya
taarifa na kupokea malamiko yaliyotokana na utekelezaji wa Operesheni
Tokomeza katika mikoa kumi na tano (15) ya Tanzania Bara ambayo ni
Kigoma, Katavi, Rukwa, Mbeya Kagera, Geita, Shinyanga, Simiyu, Mwanza
Mara,Lindi,Mtwara,Ruvuma,Iringa, Morogoro.
Pamoja na mikutano hiyo, Bw. Manyanda ametumia fursa hiyo
kuwakumbusha na kuwaomba wananchi na watanzania wa maeneo husika
kuendelea kutuma taarifa na malalamiko kuhusu utekelezaji wa Operesheni
Tokomeza kwa njia ya barua, simu na barua pepe ambapo ameeleza kuwa
wananchi wanaweza kutuma barua kwa Katibu wa Tume, Tume ya Uchunguzi wa
Operesheni Tokomeza Ujangili, SLP 9050, Dar es Salaam na barua pepe
kwenda opereshenitokomeza@agctz.go.tz.Aidha, wananchi wa maeneo husika
wanaweza kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa namba za simu za Tigo:
0714 826826; Vodacom: 0767 826826; Airtel: 0787 826826; na Zantel:
0773 826826.
No comments:
Post a Comment