Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali akichangia mjadala katika kikao cha Bunge, mjini Dodoma. Picha na Anthony Siame
Mvutano
mkali uliibuka jana bungeni wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha
Muswada wa Takwimu wa mwaka 2013, baada ya wabunge kuupinga. Muswada
huo una kipengele kinachotoa adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela na
faini isiyopungua Sh10 milioni kwa mtu au chombo cha habari
kitakachofanya makosa ya kutoa takwimu zisizokuwa sahihi.
Wabunge
hao waliufananisha muswada huo na miswada miwili ya habari ya mwaka 2015
ambayo itawasilishwa bungeni Jumanne chini ya hati ya dharura kwa usiri
uliopo na mpango wa kuiwasilisha bila wadau kushirikishwa.
Awali,
muswada wa Takwimu uliwasilishwa kwenye mkutano wa 17 wa Bunge
uliofanyika Novemba mwaka jana na wabunge wakapinga vifungu vinavyobana
waandishi wa habari kuhusu eneo la takwimu, ndipo Serikali ilipoamua
kuutoa kwa maelezo kuwa inakwenda kuurekebisha hadi ilipourejesha jana
na ukapitishwa kwa mbinde.
Jana,
Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha muswada huo, Mbunge wa Ubungo
(Chadema), John Mnyika alihoji juu ya kifungu hicho kinachotoa adhabu
kali na Serikali kujibu kuwa imeshakifanyia marekebisho.
Hata
hivyo, Mnyika hakukubaliana na maelezo hayo, bali alisema kifungu hicho
hakijafanyiwa marekebisho yoyote na Serikali na adhabu bado inaendelea
kuwa kali.
Mnyika
aliungwa mkono na mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya aliyehoji,
"Iweje Serikali iweke kinga kwa mtumishi wa Serikali anayetoa taarifa
zisizo sahihi lakini ikaacha kuweka kwa mwandishi anayepewa taarifa hizo
zisizo sahihi na ofisa huyo wa Serikali?"
Maelezo
ya Bulaya yalimfanya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju
kusimama na kusema kwa kifupi kuwa "mwandishi atakwenda kujieleza
mahakamani au polisi."
Ilivyokuwa mwaka jana
Kabla ya
kuondolewa bungeni Novemba 2014 muswada huo pamoja na mambo mengine,
ulikuwa ukipendekeza faini ya Sh10 milioni au kifungo cha mwaka mmoja
jela au vyote kwa chombo cha habari kitakachotoa taarifa za kitakwimu za
uongo au zenye upotoshaji.
"Mtu
yeyote, kwa kujifanya anatimiza majukumu yake, iwapo anapata au anaomba
kupatiwa taarifa ambayo haijaidhinishwa kuipata na kuichapisha au
kuisambaza atakuwa amefanya kosa ambalo adhabu yake ni kifungo
kisichopungua miezi 12 au faini isiyopungua shilingi milioni mbili au
vyote kwa pamoja," ilisema ibara ya 37 (d) cha muswada huo.
Muswada
huo pia ulikuwa ukiainisha kwamba takwimu rasmi ni zile ambazo
zimetolewa na kuidhinishwa na taasisi zilizoelezwa kwenye ibara hiyo ya
20 na ndizo pekee zinazoweza kutumika kama ushahidi kwenye kesi.
Adhabu
kali pia zimependekezwa kwenye muswada huo kwa vyombo vya habari ambavyo
vitatoa taarifa za takwimu zitakazosababisha watu wasishiriki kwenye
shughuli zilizoandaliwa na Serikali zinazohusiana na masuala ya takwimu.CHANZO:BBC
No comments:
Post a Comment