Nape |
Siku moja baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kusitisha
makundi yanayokwenda kumshawishi kugombea urais, Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, amempongeza kwa kutii agizo la chama hicho.
Nape amesema hatua hiyo ya Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli ni
nzuri kwa kuamua kusitisha makundi kwenda kumshawishi agombee urais,
ambayo kwa siku chache mfululizo yalikwenda nyumbani kwake Monduli na
mjini Dodoma kwa nia hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana akiwa katika ziara ya
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulahman Kinana wilayani Same, Kilimanjaro, Nape
alisema anampongeza Lowassa kwa kuwa amekubali kuheshimu kanuni,
taratibu na Katiba ya chama ambayo ndiyo inatakiwa kufuatwa na kila
mwanachama wa CCM.
Jumanne wiki hii, Nape alimuonya Lowassa kujiepusha na makundi hayo
kwa kuwa kufanya hivyo ni kukiuka kanuni na taratibu za chama na
kwamba, hali hiyo inamkosesha sifa ya kuteuliwa kugombea urais kupitia
CCM.
Nape alisema walimtaka Lowassa, ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM azuie makundi yanayokwenda nyumbani kwake
kwa ajili ya kumtaka agombee urais kwani kilichokuwa kinafanyika ni
kuanza kampeni kabla ya wakati.
“Kilichokuwa kinafanyika ni kuanza kampeni kabla ya wakati na kwa
mujibu wa chama chetu ni makosa, maana anakiuka taratibu na kanuni za
chama. Hatuwezi kukaa kimya wakati kanuni zinavunjwa wazi, hivyo
nimpongeze Lowassa kwa kutii agizo la chama,” alisema Nape.
No comments:
Post a Comment