KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

August 13, 2015

DK. MAGUFULI, LOWASSA 50/50




ZIKIWA zimesalia siku 72 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi Mkuu mwaka huu, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa nchini wanaamini kuwa hadi sasa hakuna mgombea mwenye uhakika wa ushindi wa moja kwa moja.


Wagombea wawili, Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Edward Lowassa wa Chadema ndio wanaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.


Akizungumzia uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba, aliliambia Raia Tanzania kuwa uchaguzi wa mwaka huu umethibitisha kupanuka kwa wigo wa kidemokrasia nchini.


“Hakuna anayeweza kusema moja kwa moja ni nani atakayeshinda kati ya Dk. Magufuli na Lowassa hadi sasa. Wagombea wa vyama vingine ni kama wasindikizaji tu wanaosubiri kuzigawa kura,”


“Nchi hii imebadilika tofauti na ilivyokuwa kabla ya kuvunjwa kwa Bunge la 10. Sioni kama kuna chama kitakachokuwa na kiburi kwa kingine baada ya Uchaguzi Mkuu,” alisema Kibamba.


Kibamba alisema utafiti ulioufanywa na Jukata unaonyesha hakuna uhakika wa kuwapo chama kitakachopata ushindi wa zaidi ya asilimia 60 ya wabunge.


Alisema ushindi wa asilimia 66 ndio hutengeneza theluthi mbili zinazohitajika ili chama kiwe na kiburi mbele ya vyama vingine bungeni.

Kauli hiyo ya Kibamba inapingana na kauli zilizotolewa kwa nyakati tofauti na Dk. Magufuli na Lowassa kuhusu ushindi kwenye uchaguzi huo.


Akiwa mkoani Mtwara, Dk. Magufuli aliwahakikishia wananchi kuwa ana nafasi ya kupata ushindi alioupa jina la tsunami, huku Lowassa akiwaambia mashabiki wa Ukawa kuwa yeye atashinda kwa asilimia 90 huku CCM wakiiba asilimia 10.


Akizungumzia uchakachuaji au wizi wa kura kwenye uchaguzi huo, Kibamba alisema: “Iwe CCM au upinzani, wizi wa kura utaishia kwenye kura zao za maoni ndani ya vyama vyao.


“Hakuna upande utakaothubutu kufanya hivyo safari hii. Unakumbuka mwaka jana wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa? Waliojaribu kutangaza matokeo ambayo siyo walijuta.


“Ule ulikuwa ni mwanzo tu lakini mchezo wenyewe utakuwa Oktoba mwaka huu na ieleweke kuwa ni hatari sana kwa amani ya nchi kujaribu kuchakachua matokeo.”


Kibamba alionyesha hofu kuwa safari hii si CCM pekee wanaoweza kufanya majaribio hayo, akisema mabingwa wa uchakachuaji wamegawanyika huku wengine wakiwa wamehamia upinzani.


Alisema kuhamia Chadema kwa Lowassa na wapambe wake kunafafanuliwa kama kuingia upinzani kwa mbinu zilizokuwa zikidaiwa kufanywa na CCM.


“Hoja ya pili ni kwamba walinzi wa kulinda kura hizo wakiwemo wanasiasa na watu wa usalama nao wamegawanyika; upande wa Lowassa (Chadema) na upande wa Dk. Magufuli (CCM). Nguvu zinalingana kwa hiyo safari hii patachimbika,” alisema.


Alisema ushindani wa kisiasa uliopo mwaka huu haujawahi kuonekana nchini tangu wakati wa uchaguzi maarufu wa kura tatu uliofanyika mwaka 1958 na TANU kuibuka mshindi kabla Tanganyika haijapata uhuru wake mwaka 1961.


“Watu wanauzungumzia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, lakini wakati ule unajua haikuwa rahisi kwa mtu kama mimi au wewe kukiunga mkono chama cha upinzani. Ukiwa mpinzani ulionekana kama akili yako imefyatuka.


“Wakati ule mageuzi yalikuwa hayajazoeleka, vuguvugu la uchaguzi ule haliwezi kufanana hata kidogo na uchaguzi wa mwaka huu kwa sababu safari hii hata wasomi wa juu kabisa kama maprofesa wamegawanyika, kuna waliopo chama tawala, wengine wapo upinzani.


“Wachambuzi wa masuala ya siasa nao wamegawanyika hivyo hivyo. Wasomi wamekwenda kugombea ubunge majimboni wakiwa pande zote; upinzani na chama tawala.


“Sasa hiyo maana yake ni kwamba hali inaweza kuwa kama Zambia. Awali watu walikuwa wakiona ukakasi kubadilisha chama lakini kwa hatua ilipofikia sasa, lolote linaweza kutokea,” alisema.
 
 Kura za walimu


Akizungumzia uchaguzi huo, Rais wa Chama cha Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Gratian Mkoba, alisema wafanyakazi hasa walimu wanakabiliwa na changamoto ya kupandishwa madaraja sababu inayoweza kuwafanya waamue ‘vinginevyo’ Oktoba mwaka huu.


“Wagombea itabidi wafanye jitihada kubwa kuwaonyesha Watanzania namna watakavyopambana na changamoto. Siwezi kutabiri yaliyomo kwenye vifua vya walimu, lakini hili la kutopandishwa madaraja ni suala nyeti sana kwao,” alisema Mkoba. 

Raia Tanzania.

No comments:

Post a Comment