Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
MASHEIKH saba wanaodaiwa kutoka Tanzania, wanajishughulisha na kuhubiri neno la Mungu, wanahofiwa kutekwa na kikundi cha waasi katika mji wa Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Taarifa zilizotolewa hivi karibuni, zinadai kuwa masheikh hao wanatokea Zanzibar na walikwenda nchini humo kwa ajili ya kuhubiri neno la Mungu.
Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Rajab Katimba, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwamo Serikali, wanafuatilia kwa karibu suala hilo.
Alisema masheikh hao ni miongoni mwa wanaofanya kazi bila mipaka, wakihubiri neno la Mungu mahali popote duniani.
“Tumepata taarifa ya kuwapo kwa masheikh saba ambao wametekwa na waasi nchini DRC ambao walikwenda katika mji wa Goma kwa ajili ya kuhubiri neno la Mungu.
“Masheikh hawa ni miongoni mwa makundi ya masheikh wanaohubiri neno la Mungu bila mipaka, ambao wanakwenda katika nchi mbalimbali kufanya kazi hiyo,” alisema Sheikh Katimba.
No comments:
Post a Comment