Maduka sita yanayozunguka Soko Kuu
la Morogoro, yameteketea kwa moto kutokana na hitilafu ya umeme na
kuwasababishia hasara wafanyabiashara ambayo thamani yake haijajulikana.
Mashuhuda na wamiliki wa maduka
hayo, walidai kuwa moto huo ulianzia kwenye duka la mmoja wao usiku wa kuamkia
juzi baada ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Morogoro, kurejesha
umeme na kusambaa kwenye maduka mengine.
Mmoja wa wafanyabiashara, Didas
Mushi, alilitupia lawama Tanesco kwa kuwa chanzo cha moto huo kutokana na
kukata umeme mara kwa mara na kuurejesha bila ya kutoa taarifa.
“Chanzo kwa maduka haya kuungua ni
kukatika kwa umeme wa Tanesco mara kwa mara bila kutoa taarifa na uliporudisha
majira ya saa sita usiku (juzi) ulitokea mlipuko na moto kusambaa hadi kwenye
maduka mengine,” alisema Mushi.
Mfanyabiashara wa nguo, Masanja
Okwima, alisema kuungua kwa maduka hayo kumewasababishia hasara ya zaidi ya Sh.
milioni 10 na kuitaka Tanesco kulipa gharama hizo kwakuwa wao ndio chanzo cha
moto huo.
Ofisa Uhusiano wa Tanesco Mkoa wa
Morogoro, Marcio Semfukwe, alithibitisha moto huo kusababishwa na hitilafu ya
umeme ambayo huenda imesababishwa na mmoja wa wafanyabiashara hao kuunganisha
nishati hiyo bila kibali cha shirika hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro,
Leonard Paulo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusisitiza kuwa
wanaendelea kufanya uchunguzi.
|
August 13, 2015
MOTO WAUNGUZA MADUKA MOROGORO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment