………………………………………………………………………………….
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani,
SHIRIKA la elimu Kibaha
(KEC)mkoani Pwani linatarajia kuingiza mapato ya kiasi cha sh,mil 100
kila mwaka kwa miaka 66 ijayo baada ya kuingia mkataba wa uwekezaji na
shirika la Organia kutoka Saudi Arabia na Egypt ambalo linajishughulisha
na uzalishaji kuku kwa niia ya kitaalamu.
Ujenzi wa mradi huo unatarajiwa
kukamilika mwezi Juni mwaka 2016 ambapo utagharimu fedha za kimarekani
kiasi cha sh.Milioni 60 ikiwa ni sawa na fedha za kitanzania sh.Bilioni
120.
Shirika la elimu Kibaha limeamua
kufanya jitihada za kuanzisha miradi mbalimbali kwa kushirikiana na
makampuni na mashirika mbalimbali ya ndani na nje ya nchi ili
kujiongezea mapato na kuondokana na utegemezi.
Akitoa taarifa ya shirika,wakati mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi
Evarist Ndikilo ,alipotembelea shirika hilo,mkurugenzi wa shirika la
elimu Kibaha,Cyprian Mpemba alisema miradi ndio nguzo pekee ya kuwainua
kimapato.
Mpemba alielezea kuwa shirika
limekuwa likipambana na uhaba wa fedha kutokana na kujiendesha kwa
kipindi kirefu hivyo muarobaini wa kuondokana na uhaba huo ni kuanzisha
miradi ambayo italeta tija katika shirika na wananchi wa Kibaha kijumla.
Aidha alitaja mafanikio mengine
kuwa ni wawekezaji hao kushirikiana nao kwenye shughuli za kijamii na
shirika kuongeza mapato yake kutoka sh.300,000 hadi kufikia zaidi ya sh
mil.3 kutokana na kuingia katika mfumo wa kukusanya fedha kwa njia ya
mtandao uitwao 4pay.
Mpemba alisema mapato hayo
yameongezeaka baada ya shirika kufanya uchunguzi na kubaini wizi wa
kutumia risiti na ujanja unaofanywa na baadhi ya watumishi kuliibia
shirika.
Hata hivyo alisema kwasasa
wameanza na mfumo mwingine unaoitwa GoT HoMIS Defined ambao upo chini ya
ofisi ya waziri mkuu (TAMISEMI)utakaosaidia kuongeza mapato zaid na
kugundua wizi unaofanyika kwa haraka .
Nae mkurugenzi wa shirika hilo la
kimataifa la Organia,Abdulhady Taher akielezea juu ya mradi huo
utakavyoendeshwa alisema watazalisha kuku wa aina yake Afrika Mashariki
na kutakuwa na mabanda 17 ambapo kila banda litazalisha kukuwa 35,000.
Alisema mradi huo utakapoanza
utahitaji tani 8,000 za mahindi ya njano na soya kwa ajili ya chakula
cha kuku na watahitaji yapatikane mkoani hapo na endapo hayatakuwepo
watayaagiza nje ya nchi.
Taher alisema mradi huo pia
utawezesha kupata ajira 1,200 na kipaombele chao ni kuajiri kwanza
wazawa wa Mji wa Kibaha na mkoa wa Pwani.
Aliiomba serikali kuwasaidia
upatikanaji wa umeme na maji ya uhakika kwani mradi huo ni mkubwa na
utahitaji huduma hizo kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo alisema kuwatatizo la uhaba wa ajira ambalo limekuwa likiwasumbua wakazi
wa Mji wa Kibaha na Mkoa wa Pwani kwa ujumla huenda likapatiwa
ufumbuzi mara baada ya kuanza mradi huo.
Ndikilo aliwahimiza wakazi wa mkoa huo kulima kwa wingi
mahindi ya njano ili wapate soko la uhakika katika kiwanda hicho ambacho
kitahitaji mahindi hayo na soya kwa ajili ya kuku.
Aliwaahidi wawekezaji huo
kulishughulikia suala la umeme na maji kwa kulifikisha katika wizara ama
idara husika ili lipatiwe ufumbuzi.
Mhandisi Ndikilo aliuambia
uongozi wa shirika hilo kuwa ni vyema suala la kupatikana mwenyekiti wa
bodi ya shirika la elimu likashughulikiwa kwani ni muda mrefu shirika
hilo halina mwenyekiti ambae watashirikiana nae kusukuma maendeleo ya
shirika.
Alilipongeza shirika kwa hatua
wanazozichukua za kimaendeleo na kutokana na mambo mazuri yanayofanyika
ataangalia uwezekano wa kuomba mh.Rais wa jamhuri ya muungano wa
Tanzania Dk Jakaya Kikwete wakati wa ziara ya kuwaaga wakazi wa mkoa huo
utengwe muda wa kutembelea miradi hiyo ili atambue anauacha mkoa ukiwa
umepiga hatua.
Shirika la elimu Kibaha
lilianzishwa mwaka 1970 ambapo miaka ya 60 lilikuwa likiongozwa na nchi
za Nordic ikiwemo nchi ya Norway na Dermark ,na lina ardhi yenye ukubwa
wa hekta 1,357.
No comments:
Post a Comment