Patricia Kimelemeta na Grace Shitundu, Dar es Salaam
ZIKIWA zimebaki siku chache kabla ya kuanza kampeni za wagombea urais, wabunge namadiwani nchini, leo wagombea hao wanatarajiwa kurudisha fomu zao kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Wagombea wawili wa urais ambao wamekuwa na nguvu katika kinyang’anyiro hicho, Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Edward Lowassa anayewakilisha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), watarudisha fomu za kuwania nafasi hiyo huku Jeshi la Polisi likiwa limepiga marufuku mbwembwe na maandamano kwa wafuasi wa vyama vya siasa.
Kutokana na zuio hilo, wagombea hao ambao wamekuwa gumzo katika duru za siasa nchini watarudisha fomu kimya kimya huku wakisubiri uzinduzi rasmi wa kampeni, kwa mujibu wa ratiba za vyama vyao.
Urejeshaji huo wa fomu unakamilisha siku kadhaa ambazo wagombea hao walitafuta wadhamini mikoani kama ilivyo katika mahitaji ya Sheria ya Uchaguzi.
Wakati kampeni zikitarajiwa kufunguliwa kesho baada ya kukamilika kwa uteuzi wa NEC, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya mwavuli wa Ukawa kikiwa bado hakijataja tarehe ya uzinduzi kwa mgombe urais wake, hali ni tofauti kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho Jumapili Agosti 23 mwaka huu kitazindua kampeni zake katika Uwanja wa Jangwani.
Kuanza kwa kampeni hizo ni mwanzo wa siku 70 za kampeni kwa wagombea wa vyama 13 waliochukua fomu ya kuwania nafasi hiyo kubwa nchini.
Baada ya kumaliza hatua ya kutafuta wadhamini, wagombea hao walitakiwa kusaini hati ya kiapo mahakamani kwa jaji waweze kukidhi vigezo vya kuwania nafasi hiyo.
RATIBA YA NEC LEO
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), mgombea urais wa chama cha UPDP, Fahmi Dovutwa atarudusha fomu saa 3.00 asubuhi, akifuatiwa na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), Edward Lowassa saa 4:00 asubuhi huku Dk. John Magufuli wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akitarajiwa kuwasilisha fomu zake saa 5:00 asubuhi.
Ratiba hiyo pia inaeleza kuwa Chama cha Wakulima (AFP) saa 5:00, Maximilian Lyimo (TLP) saa 6:30, Chifu Lutalosa Yemba (ADC) saa 7:00, ACT- Wazalendo 7:30, NRA saa 8:00, CHAUMMA saa 8:30, Godgrey Malisa (CCK) saa 9:00, DP saa 9:00 na TADEA saa 9:30.
No comments:
Post a Comment