Huduma za kupima shinikizo la damu zikiendelea |
Dawati la elimu kwa Umma likiwa kazini |
……………………………………………………………………………….
Na Grace Michael, Arusha
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya
umeombwa kutekeleza zoezi la upimaji wa afya za wananchi katika
Halmashauri zote nchini ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu ya namna ya
kuepukana na magonjwa hayo ili kuliwezesha Taifa kuwa na wananchi wenye
afya imara.
Rai hiyo imetolewa na watumishi
mbalimbali katika mkutano wa kwanza wa mwaka wa Serikali Mtandao
uliofanyika mkoani hapa ambapo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ulitoa
huduma za upimaji afya bure katika magonjwa yasiyoambukiza.
Akizungumzia hilo, Godfrey Luguma
kutoka Halmashauri ya Wilaya Munduli alisema kuwa ni vyema NHIF ikawa
na ratiba ya kuzunguka katika maeneo yote ili fursa hii iwafikie
Watanzania wote.
“Upimaji na uhamasishaji wa
wananchi kujiunga na Mifuko hii ikiwemo ya Afya ya Jamii iendelee ili
kila mwananchi aweze kutambua hali ya afya yake hatua itakayomuwezesha
kuwa na mipango imara ya kimaendeleo,” alisema Bw. Luguma.
Naye Nkide Mwaikuka kutoka
Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa alitoa mwito kwa wananchi kuhakikisha
wanajiunga na utaratibu wa bima ya afya ili wawe na uhakika wa kupata
matibabu wakati wote.
“Bima ya Afya ni mpango mzuri
sana kwa watumishi wa umma na hata wananchi wa kawaida, hivyo NHIF
ongezeni elimu kwa wananchi hususan vijijini ili watambue umuhimu wa
kuwa au kutumia mpango huu,” alisema Bw. Mwaikuka.
Aidha washiriki wengine wametumia
fursa hiyo kupima afya zao huku wakiupongeza Mfuko kwa kuanzisha zoezi
hilo kwa lengo la kuhakikisha afya za watanzania zinabaki kuwa bora.
Akizungumzia rai iliyotolewa ya
upimaji ndani ya halmashauri zote, Mkurugenzi wa Mifumo Habari wa NHIF,
Othman Ali alisema kuwa mpango huo unafanyika katika maeneo mengi ya
nchi hii hivyo akawaomba wananchi kutumia fursa hizo wakati zinapokuwa
zimejitokeza.
“Tunazo ofisi katika kila mkoa
ambazo zinafanya haya majukumu kupitia mpango wa Elimu ya Kata kwa Kata
ambapo zoezi la upimaji wa afya kwa wananchi hufanyika,” alisema Bw.
Othman.
No comments:
Post a Comment