Kikosi
cha Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kimeanza mazoezi katika uwanja wa
Karume kujiandaa na mchezo dhidi ya Nigeria kuwania kufuzu kwa Fainali za
Mataifa ya Afrika mwaka 2017 nchini Gabon.
Wachezaji
wa Taifa Stars chini ya kocha wake mkuu Charles Mkwasa watakua wakijifua mara
mbili kwa siku asubuhi na jioni katika uwanja wa Karume katika kujiweka fit na
maandalizi ya mchezo huo.
Kufuatia
baadhi ya wachezaji kuwa na majukumu na timu zao kujiandaa na mchezo wa Ngao ya
Hisani utakaochezwa Agosti 22, Mkwasa amewaongeza wachezji wengine kumi (10)
kutoka katika orodha yake ya akiba.
Lengo
la kambi hii ya awali ya siku tano, ni kocha mkuu pamoja na benchi lake la
ufundi kupata nafasi ya kuwaona wachezaji katika mazoezi hayo kabla ya safari
ya kuelekea nchini Uturuki Agosti 23 mwaka huu kwa kambi ya siku kumi.
Wachezaji
walioitwa na kuanza mazoezi leo ni Said Mohamed, Vicent Andrew (Mtibwa Sugar),
Mohamed Hussein, Ibrajim Hajibu (Simba SC), Hamis Ali, Juma Mbwana (KMKM),
Tumba Sued (Coastal Unioni), Samuel Kamuntu (JKT Ruvu), Ibrahim Hilka
(Zimamoto– Zanzibar) na Mohamed Yusuf (Prisons).
Wachezaji wengine waliopo kambini ni Said Ndemla, Hassan
Isihaka, Abdi Banda(Simba SC), Rashid Mandawa (Mwadui FC), Michael Aidan (Ruvu
Shooting), Orgeness Mollel (Aspire Academy) na Abdulhaman Mbambi (Mafunzo).
TWIGA
STARS KUIVAA HARAMBEE STARLETS
Timu ya Taifa ya Tanzania
ya Wanawake (Twiga Stars) iliyopo kambini kisiwani Zanzibar, inatarajiwa
kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya taifa ya Wanawake kutoka Kenya (Harambee
Starlets) Agosti 23, 2015.
Mchezo huo wa kirafiki utachezwa katika uwanja wa Aman Kisiwani
Zanzibar, ikiwa ni sehmu ya maandalizi ya kikosi hicho kujiandaa na fainali za
Michezo ya Afrika (All Africa Games) zitakazofayika nchini Congo-Brazzavile
kuanzia Septemba 4 – 19, 2015.
Twiga Stars inaendelea na mazoezi kutwa mara mbili katika
viwanja vya Aman na Fuoni chini ya kocha wake mkuu Rogasian Kaijage kujiandaa
na fainali hizo za michezo ya afrika, wachezaji wote waliopo kambini wapo
katika hali nzuri wakiendelea kujifua na michezo ya Afrika.
USAJILI Dirisha la usajili limeongezwa toka
tarehe 06 Agosti hadi tarehe 20 Septemba, baada ya muda huo klabu
itakayochelewesha kuleta usajili wake itatozwa kiasi cha shilingi laki tano
(Tsh 500,000) kwa kila mchezaji itakayemsajili mpaka siku ya tarehe 30 Agosti.
Mwisho wa kufanya uhamisho wa
kimataifa wa wachezaji kwa njia ya mtandao TMS ni tarehe 6 Septemba.
Kikao cha kamati ya sheria kitakaa
tarehe 28 kwa ajili ya kuupitisha usajili na kitakaa tena tarehe 8/9/2015 kwa
ajili ya kupitisha usajili.
Kuanzia tarehe 21 hadi 27 itakuwa ni
wiki ya pingamizi, ambapo majina yatabandikwa TFF Karume na kuwekwa kwenye
mtandao ili kuwezesha vilabu vyenye pingamizi kuwawekea wachezaji mapingamizi.
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inatarajiwa
kuanza tarehe 12 Septemba 2015, Daraja la kwanza (FDL) ikitarajiwa kuanza
Septemba 17 na Ligi Daraja la pili inatarajiwa kuanza Oktoba 16 mwaka huu.
MICHUANO YA COPA
COCA-COLA 2015
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) bado linaendelea na mazungumzo na wadhamini wa michuano hiyo (Coca-Cola).
Kutokana na mazungumzo hayo, ratiba ya michuano hiyo itachelewa kutoka.
Hivyo, tunawaomba kuwa na uvumilivu
wakati mchakato wa mazungumzo hayo yanayokaribia ukingoni ukiendelea.
UAMUZI WA KAMATI YA RUFAA YA TFF JUU YA RUFAA YA DR. DEVOTA
JOHN MARWA,YA MAAMUZI YA KAMATI YA UCHAGUZI WA SOKA LA WANAWAKE (TFF)
Mwomba rufani, Dr. Devota John
Marwa, (Mrufani) ni msomi mbobezi katika taaluma ya michezo, akiwa ni mhadhiri
katika kitengo kinachojihusisha na taaluma ya michezo katika Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam. Akiamini kwamba anakidhi vigezo vilivyowekwa kwa nafasi ya mgombea
uenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake(TWFA), alichukua fomu ya kuomba
kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama hicho.
Maombi hayo yalikumbana na pingamizi
zilizoletwa na wakereketwa wawili wa soka la Wanawake, Bi. Chichi Mwidege na
Bi. Mwajuma Noty, ambao kwa pamoja walimwekea pingamizi Mrufani, kwamba hakidhi
matakwa ya kanuni za ugombea wa nafasi ya Mwenyekiti.
Waleta mapingamizi walidai kuwa
Mrufani hakuwa na sifa zilizoainishwa katika Kanuni za Uchaguzi za T.F.F. (TFF
Electoral Code) Ibara ya 9 (tisa) kipengele cha 3 (tatu), kinachomtaka mgombea
awe amejihusisha na uongozi wa mpira wa miguu kwa muda usiopungua miaka mitano.
Aidha Ibara ya 28 (ishirini na nane)
kipengele cha 3 (tatu), kinamtaka mgombea awe amejihusisha japo miaka 2
(miwili) katika shughuli za maendeleo ya mpira wa miguu nchini. Kamati ya Uchaguzi iliridhia mapingamizi hayo
na kuliondoa jina la Mrufani katika orodha ya wagombea wa nafasi hiyo ya
Mwenyekiti. Rufani hii ni matokeo ya uamuzi huo wa Kamati ya Uchaguzi
uliotolewa taraehe 22 Julai, 2015.
Kwa ujumla, sababu za kupinga
maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi zinaweza kuhesabiwa kuwa ni mbili. Moja ni
iliyojikita juu ya hitilafu katika kuamua kwamba Mrufani hakuwa na uzoefu
katika uongozi wa soka kwa muda ulioainishwa. Sabau nyingine ni kwamba Kamati
ya Uchaguzi illibua sababu ambayo haikuwa katika Hati ya pingamizi iliyoletwa
na Mleta pingamizi.
Wakati ambapo Mleta pingamizi alijikita katika
kipengele cha 28(3), Kamati iliibua kipengele cha 28(8), cha Katiba ya TWFA
kinachomtaka mgombea awe ametimiza uzoefu wa uongozi wa miaka mitano, ambacho
hakikuwemo katika hoja za pingamizi zilizowasilishwa na mleta pingamizi.
Katika kufikia uamuzi wake, Kamati
ya Rufani ilizipitia sababu za Mrufani kama zilivyoletwa, na baada ya
kusikiliza maelezo ya Mrufani na hoja za Mwakilishi wa TFF, Wakili Msomi Edward
Augustino, na imeamua kama ifuatavyo. Tutaanza na hoja ya mwisho.
Je, Kamati ilikuwa sahihi kuibua
kipengele ambacho hakikuletwa katika hati ya mapingamizi? Kamati inaweza kuibua
kipengele hicho endapo kwa kufanya hivyo, itakuwa imejielekeza katika nia njema
ya maslahi ya suala linalozungumziwa.
Sharti jingine ni kwamba hoja hiyo
inyoibuliwa isiwe na athari hasi(prejudicial) kwa mhusika. Kaika suala hili
hata hivyo, hoja iliyoletwa na Mleta pingamizi, yaani hoja chini ya kifungu cha
28 (3), imeainisha kipindi kifupi cha uzoefu
(miaka 2), na hoja iliyoibuliwa na
Kamati inahitaji uzoefu wa miaka 5.
Endapo Mrufani angekuwa na uzoefu wa
miaka 3 hadi 4, bado angekwama kutokana na hoja iliyoibuliwa na Kamati. Hii kwa
vyovyote ingekuwa ni athari hasi (negative impact) katika harakati za Mrufani.
Ni vema
Kamati zinazosikiliza malalamiko
zikajikita kwenye malalamiko yaliyoletwa na wahusika wenyewe. Kama pigamizi
lingekuwa liko juu ya kipengele hicho tu, tusingesita kukubaliana na sehemu hii
ya rufani. Hata hivyo, takwa la uzoefu wa miaka 5 limeainishwa pia katika Ibara
ya 9 (3), ambayo ilikuwa ni sehemu ya mapingamizi yaliyokuwepo kwenye hati ya
mapingamizi.
Kwa sababu hiyo, Kamati ya Rufani
haioni kama hoja hiyo ina mashiko. Haitaitilia maanani. Hoja kuu ndani ya rufaa
hii ni je, Kamati ya Uchaguzi ilijielekeza vema kuhusu suala la uzoefu wa
uongozi ulioainishwa na Katiba?
Mrufani ameieleza Kamati ya Rufani
mlolongo wa shughuli ambazo amekuwa akizifanya, nyingi zikiwa zimejikita zaidi
katika taaluma. Miongoni mwa shughuli hizo ni kuandaa Mpango Mkakati wa
kuendeleza soka la wanawake. Mpango huu uliridhiwa na kuwasilishwa Makao Makuu
ya Shirikisho la Mpira Duniani, yaani FIFA.
Maelezo mengine ni kushiriki katika
kuongoza timu mbali mbali kule Chuo Kikuu, zingine zikiwa za watoto wadogo
ambao baadhi ya matunda yake ni wachezaji walioibukia kwake kama vile Simon
Msuva. Alisema zaidi kuwa alishiriki kuandaa warsha ilizoandaliwa kwa
ushirikiano kati ya FIFA na TFF.
Aidha. Alisema kuwa amekuwa kiongozi
tangu akiwa bado kwenye vyuo vya ualimu, na baadaye alipohitimu na kufanya kazi
kama Mwalimu, kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliko mpaka
sasa. Akasema, hata alipokuwa Sweden kwa masomo ya juu pia lijihusisha na
programu za maendeleo ya soka la wanawake.
Wakili msomi wa TFF akijibu hoja
hizo, alikubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi kuwa Mrufani hajaonesha
popote kwamba amewahi kuongoza soka, akasema Mrufani ni mtaalamu tu kama msomi,
jambo linaloweza kufanywa na msomi yoyote. Akamalizia kwa kuiomba Kamati ya
Rufani za Uchaguzi kuitupilia mbali rufaa ya Mrufani kwa kukosa mashiko.
Tofauti na Kamati ya Uchaguzi,
Kamati ya Rufani imeona kuwa kwa maslahi mapana ya mchezo wa soka katika ujumla
wake, ni vema kuweka tafsiri pana (wide interpretation) juu ya sifa
zinazozungumzwa, badala ya kuweka tafsiri finyu (restricted/narrow
interpretation) kama ilivyofanya Kamati ya Uchaguzi.
Baada ya kufanya hivyo, kuhusiana na
Mrufani, Kamati imeona kuwa ana sifa zinazostahili. Kupitia sababu alizozitoa,
na vielelezo vyake, Kamati ya Rufani haina wasiwasi kuwa Mrufani ana uzoefu
mbali mbali sio katika soka tu, bali pamoja na michezo katika ujumla wake.
Tumeshuhudia katika maelezo yake
kwetu kwamba ushiriki wake katika hatua mbali mbali, japo hakuwahi kuchaguliwa,
sio ushiriki wa kitaaluma tu, kama msomi mwingine yeyote. Ni ushiriki wenye
dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko/maendeleo katika soka la wanawake.
Maelezo
yake kuwa aliaandaa programu ya
maendeleo ya soka la wanawake, hayakupingwa. Kamati ya Uchaguzi ingeangalia
namna ambavyo “visheni” iliyomo katika programu ile ambavyo ingeweza
kutekelezwa na mtu aliyeaiandaa. Kwa hiyo, katika hoja hii, Kamati inakubaliana
kuwa Mrufani
anazo sifa stahiki, na kukatwa kwa
sababu hii, Kamati ya Uchaguzi haikujielekeza vema. Kwa hiyo, Mrufani ameshinda
rufaa yake? Kamati ya Rufani inachelea kujibu swali hili moja kwa moja.
Utaratibu wa kuwasilisha rufani ulikiukwa, na hapa ndipo rufaa hii inapokwaa
kisiki. Chini ya Ibara ya 13 (1) cha
Kanuni ya
Uchaguzi (Electoral Code), mgombea
ambaye hakuridhika na maamuzi, atawasilisha rufaa yake ndani ya siku 3 (tatu)
tangu uamuzi anaoupinga ulipotolewa.
Kipengele cha 3 (tatu) cha ibara
hiyo kinasema kwamba Mrufani yoyote atakuwa na uhalali endapo rufaa yake
imewasilishwa kwa mujibu wa kanuni hizo.
Uamuzi unaolalamikiwa ulitolewa tarehe 22 Julai 2015, sababu za rufaa
ziliandaliwa tarehe 27 Julai na sababu hizo za rufaa zililipiwa tarehe 28
Julai, 2015. Ni dhahiri kwamba rufaa ililetwa nje ya muda uliowekwa na kanuni,
na kwa hiyo inakosa uhalali kisheria na kikanuni.
Japo katika mwenedo na maamuzi yake
Kamati ya Rufani za Uchaguzi haifungwi na taratibu za kimahakama, suala la muda
wa kuwasilisha rufani sio miongoni mwa mambo ambayo Kamati inaweza
kutoyazingatia. Kwa sababu hiyo, Rufaa hii imetupwa, lakini kwa sababu tofauti
na zile za Kamati ya Uchaguzi.
Pamoja na uamuzi huu, Kamati ya
Rufani za Uchaguzi inapenda kwa namna ya kipekee kumpongeza Mrufani kwa
jitihada alizozionesha kutaka kuitumikia TWFA. Ni matumaini ya Kamati kuwa
hatokata tama, na kwamba atakuwa tayari, akitakiwa kufanya hivyo, kupitia
taalum yake, kushirikiana na wenzake katika jitihada za kuendeleza soka la
akina mama lililo na changamoto lukuki.
Imetolewa na,
JULIUS M. LUGAZIYA
Mwenyekiti-Kamati ya Rufani za
Uchaguzi
IMETOLEWA
NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment