Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amesema nchi za Afrika
haziwezi kukwepa misaada kutoka nchi za Ulaya kwa kuwa misaada hiyo ni
jukumu lao la kihistoria.
Kikwete alisema hayo jana wakati wa
ufunguzi wa mkutano wa siku mbili unaojadili malengo mapya 17 ya Umoja
wa Mataifa yanayohusu ‘Maendeleo Endelevu kwa mwaka 2030’.
Mkutano
huo umejikita kujadili lengo namba 16 linalohimiza haki, amani na jamii
shirikishi, hasa katika masuala ya utawala wa sheria kama chachu ya
maendeleo endelevu.
Kikwete alisema jukumu hilo linapaswa
kuendelezwa kwa kuwa maendeleo ya nchi za Ulaya yalitokana na rasilimali
walizozitoa Afrika kipindi cha ukoloni.
Alisema nchi za Afrika
zina rasilimali za kutosha hivyo, ili zifanye kazi bado kunahitajika
uwekezaji ambao utaweza kuinua viwanda na kukuza uchumi wa nchi za
Afrika, kwani bila hivyo itachukua muda mrefu kufika mbali kiuchumi.
Hata
hivyo, alisema nchi za Afrika lazima zijiwekee utaratibu wa namna ya
kupokea misaada hiyo, lakini lengo liwe ni kunufaisha wazawa na kwa
kufuata sheria za nchi husika na zile za kimataifa.
“Misaada
tunayoizungumzia siyo lazima iwe fedha, bali tunahitaji wawekeze zaidi
kwetu kwa mikataba ya kisheria inayolinda wazawa, kwa mfano Tanzania
tuna rasilimali za kutosha kama gesi, madini na vinginevyo, lakini hivi
vyote vinahitaji kuibuliwa na kutayarishwa. Lazima tuwape nafasi ili
kufanikisha lakini kwa sheria zitakazowalinda Watanzania,” alisema
Kikwete.
Kauli hiyo ya Kikwete imekuja wakati Rais wa Awamu ya
Tano, John Magufuli amekwisha kuweka msimamo katika hotuba zake kadhaa
akitaka Tanzania ijitegemee kwa asilimia kubwa badala ya kutegemea
misaada ya nje.
Wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa
barabara ya kwanza ya juu (flyover) katika makutano ya Barabara za
Mandela na Nyerere eneo la Tazara, Rais Magufuli aliita misaada ya
wahisani ‘mkate wa masimango’ na kusema kuliko kula mkate huo ni bora
kushindia muhogo.
Ingawa hakufafanua wala kuzungumza kwa undani
juu ya kauli hiyo, lakini aliitoa ikiwa zimepita siku chache tangu
Shirika la Maendeleo la Milenia (MCC) la Mareka ni kusitisha msaada wa
Dola za Marekani milioni 472.8 karibu Sh1 trilioni kwa madai kuwa
Tanzania ilikiuka misingi ya kidemokrasia kwa kurudia uchaguzi wa
Zanzibar na kushindwa kusimamia She ria ya Makosa ya Mtandao.
Pia,
Rais Magufuli Machi 29, akiwa katika kijiji cha Mlimani, Wilaya ya
Chato mkoani Geita alisema jukumu kubwa lililo mbele ya Watanzania kwa
sasa ni kushikamana na kujisimamia katika maendeleo ili kila mmoja
ahakikishe anaongeza uzalishaji na utendaji kazi mahali pake pa kazi.
“Kwa
hiyo ni lazima tujisimamie sisi wenyewe, na tukijisimama sisi wenyewe
kwa kila mmoja kuwajibika mahali alipo, kama ni mfanyakazi afanye kazi
kwelikweli, kama ni mkulima afanye ukulima wake kwelikweli, kama ni
mfanyabiashara afanye biashara kwelikweli, kama ni mfugaji afuge
kwelikweli, kama ni mvuvi avue kwelikweli, Tanzania hii tutavuka,”
alisema.
Mkutano huo ulioandaliwa na Taasisi ya Kimataifa ya
Maendeleo ya Sheria (IDLO) yenye makao makuu yake nchini Italia, ambayo
kwa Tanzania mlezi wake ni Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin
Mkapa.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mkapa alisema katika nchi
yeyote ili kupata maendeleo ni lazima kuwe na Katiba ya wananchi ambayo
haitalenga kundi moja.
“Awali nchi nyingi za Afrika hazikuwa na
Katiba ya wananchi, bali kulikuwa na Katiba ya chama ambayo kwa sasa ni
nchi za kidikteta pekee zimebaki na mfumo huo, kwa sasa tulilenga
kuweka sera, mikakati thabiti ili tuweze kutekeleza malengo mapya ya
dunia chini ya dira mpya ya Umoja wa mataifa ya maendeleo ya dunia,”
alisema Mkapa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na
Utawala Bora, Angela Kairuki alisema kama ilivyo ajenda ya nchi za
Afrika, nchi haiwezi kuwa na utawala wa sheria kama hakuna upatikanaji
mzuri wa sheria.
“Lazima uweke mifumo mizuri ya kutatua migogoro
pia, utoaji wa vibali bila kutoa rushwa, hata katika uwekezaji
utakapokuwa huna sheria nzuri inayolinda upande huo ni vigumu wawekezaji
kuwepo,” alisema Kairuki.
Mkurugenzi Mkuu wa IDLO, Irene Khan alisema mkutano huo umejikita katika kujadili haki, amani na jamii shirikishi.
“Lengo
ni kuwa na dira mpya ya maendeleo ya dunia inayolenga kutokomeza
umaskini, kulinda mazingira, kupambana na mabadiliko ya tabianchi na
kushirikisha makundi yote kwenye jamii katika masuala ya maendeleo,”
alisema Khan.
|
June 2, 2016
KIKWETE:NCHI ZA AFRIKA HAZIWEZI KUKWEPA MISAADA YA WAZUNGU
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment