Serikali
imewasilisha miswada miwili ya marekebisho ya sheria mbalimbali ya
mwaka 2016 ikiwamo ya kuanzishwa kwa Mahakama Maalumu ya Rushwa.
Watakaokutwa na hatia ya makosa ya rushwa au uhujumu uchumi, watafungwa kifungo kisichopungua miaka 20 na kisichozidi miaka 30.
Kuanzishwa
kwa mahakama hiyo ni kutimiza ilani ya CCM na ahadi ya Rais John
Magufuli kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana kuwa ataianzisha ili
kushughulika na mafisadi pamoja na wahujumu uchumi.
Kwa
mujibu wa muswada huo, mahakama hiyo inaanzishwa katika marekebisho ya
Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 yatakayo fanyika katika Kifungu cha
3.
“Lengo
la marekebisho hayo ni kuanzisha Divisheni ya Mahakama Kuu ya Makosa ya
Rushwa na Uhujumu Uchumi itakayokuwa na mamlaka ya kusikiliza na kuamua
mashauri yanayohusiana na makosa ya rushwa na uhujumu uchumi, ambayo
itakuwa na mamlaka ya kusikiliza mashauri yenye thamani isiyopungua Sh1
bilioni,” unaeleza muswada huo uliowasilishwa kwa mara ya kwanza bungeni jana.
Mbali na makosa hayo, pia mahakama hiyo itashughulika na makosa ya uhujumu uchumi bila kujali thamani yake.
Katika sheria hiyo, yatafanyika marekebisho mengine yanayohusu muundo, mamlaka na utekelezaji wa mahakama inayopendekezwa.
Pia
masuala ya kuzuia ufilisi, mamlaka ya Jaji Mkuu kutengeneza kanuni na
makosa ya rushwa na uhujumu uchumi, ni mambo yaliyozingatiwa katika
marekebisho hayo.
Muswada
huo umeeleza kuwa masharti yaliyomo kwenye Sheria ya Usalama wa
Mashahidi, Sura ya 446 yanapendekezwa kutumika katika masuala
yanayohusiana na usalama wa mashahidi kwa kukifanyia marekebisho kifungu
cha 53.
Masuala
mengine yanayopendekezwa yanahusu utaratibu wa kuwafikisha watuhumiwa
mahakamani, utoaji wa dhamana na adhabu, pamoja na utaratibu wa kukata
rufaa.
“Taratibu
nyingine za uendeshaji na utekelezaji wa masharti ya sheria hii itakuwa
kama itakavyofafanuliwa katika kanuni zitakazoandaliwa na Jaji Mkuu,” umeeleza mswada huo.
|
June 2, 2016
SHERIA YA MAHAKAMA YA MAFISADI YATINGA RASMI BUNGENI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment