Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha sherehe za
kuadhimisha miaka 50 tangu Benki Kuu ya Tanzania ilipoanzishwa.
Sherehe hizi zitafanyika katika
Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam tarehe
22/06/2016 ambapo mgeni rasmi atazindua vitabu viwili na kufuatiwa na
kongamano litakaloshirikisha wataalam mbalimbali wa uchumi wakiwemo
magavana 20 wa benki kuu kutoka nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Mada kuu katika Kongamano hilo
itakuwa: “Beyond Aid and Concessional Borrowing: New Ways of Financing
Development in Africa and its Implications”, (yaani namna ya kupata
fedha za miradi ya maendeleo zaidi ya misaada na mikopo nafuu na athari
zake) itakayowasilishwa na Prof. Justin Lin wa Chuo Kikuu cha Peiking,
China. Mada hii imechaguliwa kwa kuzingatia changamoto ambazo serikali
za Afrika zinakumbana nazo katika kugharamia miradi ya maendeleo wakati
ambapo misaada na mikopo nafuu imekuwa ikipungua kwa kiasi kikubwa.
Wachumi waliobobea wa ndani na
nje ya nchi, wakiwemo magavana 20 kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika
mashariki (EAC) na wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika
(SADC) watashiriki katika kongamano hilo.
Vitabu vitakavyozinduliwa siku
hiyo ni (i) “Tanzania: The Path to Prosperity” kinachoelezea masuala
yanayohusu sera za uchumi nchini Tanzania ambacho kimeandikwa na wachumi
waliobobea wa ndani na nje ya nchi, na kimechapishwa na Oxford
University Press. (ii) Kitabu cha pili ni cha miaka 50 ya Benki Kuu ya
Tanzania kiitwacho “50th Anniversary of the Bank of Tanzania:
Evolution of the Bank of Tanzania’s Role and Functions”, ambacho
kinaelezea historia, majukumu, mafanikio na changamoto za Benki Kuu
katika kipindi cha miaka 50 na matarajio ya Taasisi hii ya Umma katika
maendeleo ya taifa katika kipindi cha miaka 50 ijayo.
Aidha, Tarehe 11/6/16 Mheshimiwa
Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa atakuwa Mgeni Rasmi kwenye
matembezi ya hisani ya wafanyakazi wa Benki Kuu kutoka makao makuu ya
Benki hadi viwanja vya Mnazi Mmoja kuchangia ununuzi wa madawati ya
shule za msingi kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Benki.
Wafanyakazi wa Benki Kuu walioko matawini Mtwara, Mwanza, Dodoma,
Arusha, Mbeya, Zanzibar na Chuo cha Benki Mwanza nao pia watafanya
matembezi ya hisani kwenye mikoa yao.
Pamoja na matembezi kutakuwa na
maonesho yaliyoandaliwa na Benki Kuu katika viwanja vya Mnazi Mmoja
yenye lengo la kuwapa wananchi historia ya taasisi hii, ilikotoka, ilipo
na inakoelekea katika kutekeleza majukumu yake.
Benki Kuu ingependa kuwakaribisha
wananchi kufika kwa wingi kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja siku hiyo ya
tarehe 11/6/16 kujifunza mengi kuhusu taasisi hii ya umma.
Aidha, tunawaomba wananchi
kufuatilia vipindi mbalimbali vya redio na makala kwenye magazeti ambapo
mengi kuhusu historia, changamoto, mafanikio na matarajio ya Benki
yataelezwa na viongozi mbalimbali wa Benki wa sasa na waliopita.
Benki Kuu ilianzishwa kwa mujibu
wa Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 1965 na kuanza kutoa huduma rasmi tarehe
14 mwezi Juni mwaka 1966. Katika kipindi cha uhai wake, Benki Kuu ya
Tanzania imetimiza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kulingana na
mahitaji ya taifa yalivyojitokeza mwaka hadi mwaka.
Imetolewa na:
Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki
03/06/2016
|
No comments:
Post a Comment