Naibu
Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson sasa amesababisha makubwa zaidi;
wabunge kutoka vyama vya upinzani wako radhi kutimuliwa wote iwapo
kiongozi huyo ataongoza vikao vyote vilivyosalia na wao kuendelea na
msimamo wao wa kumsusia.
Jana,
Dk Ackson aliingia kuongoza kipindi cha maswali na majibu na wabunge
wote wa vyama vya upinzani wakatoka ndani ya ukumbi na alipomuachia
mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kuendelea na shughuli zilizosalia,
walirejea ukumbini.
“Kama
Naibu Spika atakuwepo kwenye kile kiti, hatatuona bungeni, hata kama ni
leo, ni kesho hata Bunge lote. Tuko tayari kuchukua gharama hiyo,”
alisema kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe akiwa nje ya
ukumbi wa Bunge baada ya kuongoza wabunge wenzake kutoka ukumbini wakati
wa kipindi cha maswali na majibu.
Kauli
hiyo ya Mbowe imekuja siku moja baada ya Dk Ackson kukataa Bunge
kujadili sakata la wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom)
waliotimuliwa kwa maelezo kuwa hawafundishwi kwa muda mrefu kutokana na
walimu wao kugoma wakidai malimbikizo yao.
Kitendo
cha Dk Ackson kukataa hoja hiyo ijadiliwe, kilisababisha vurugu bungeni
kiasi cha kuita askari kuingia kuwatoa wabunge waliokuwa wakipiga
kelele na baadaye kuwaamuru waliokataa kukaa waondoke ukumbini.
Wakiwa
nje, walifikia uamuzi wa kususia vikao vyote vitakavyoongozwa na Naibu
Spika na wakaanza kutekeleza uamuzi huo jana asubuhi.
Kauli
ya Mbowe pia imekuja siku moja baada ya Kamati ya Maadili, Kinga na
Haki za Bunge kuwasimamisha wabunge saba kutoka vyama vya upinzani
kuhudhuria vikao vya kuanzia mkutano huu hadi ujao kwa maelezo kuwa
walifanya fujo wakati wakipinga hoja ya Serikali ya kusimamisha
matangazo ya moja kwa moja ya baadhi ya shughuli za Bunge.
Jana,
Mbowe alisema wako tayari kutimuliwa wote kama uamuzi huo utawapendeza
viongozi wa Bunge kwa kuwa siasa inaweza kufanywa ndani na nje ya
Bunge.
Mbowe
alisema kuwa hali ilishafika hatua nzuri ya kujenga demokrasia nchini
na kwamba pamoja na matatizo yaliyokuwepo, hali ilikuwa ikienda vizuri.
“Lakini
tangu kuingia kwa Serikali ya Awamu ya Tano mnaweza kuona Bunge
limegeuka kituko. Bunge limegeuka mahali pa kukomoana. Bunge limekuwa
mahali pa kutishana,” alisema Mbowe.
“Naibu Spika anaamua kusitisha mjadala wa maana ili apate muda wa kuwadhibiti na kuwafukuza wabunge bungeni na anaona sifa.
Tunaacha
kujadili hoja ya msingi kama mambo ya Udom. Watoto wadogo wanalala nje
haoni ni muhimu, anaona muhimu ni kuwafukuza wabunge wa upinzani.”
Mbowe, ambaye pia ni mbunge wa Hai, alisema hawezi kukaa, kumsikiliza na kumheshimu Dk Ackson, bali wapinzani wataheshimu anayewaheshimu bila kujali anatoka chama gani na hawatamuheshimu asiyewaheshimu bila kujali cheo chake.
“Sasa
leo (jana) tumekataa kushiriki kipindi cha maswali na majibu kwa sababu
yeye (Dk Ackson) anasimamia kipindi hicho na akitoka tutarudi bungeni.
Akija
mwenyekiti, akija Spika mwenyewe tutarudi bungeni. Lakini kama Naibu
Spika atakuwepo kwenye kile kiti hatatuona bungeni, hata kama ni leo, ni
kesho hata Bunge lote. Tuko tayari kuchukua gharama hiyo,” alisema Mbowe.
Dk Ackson alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanzia Septemba mwaka 2015 hadi Novemba 2015 alipochukua fomu za kugombea uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya CCM.
Siku
moja kabla ya CCM kuchagua mgombea wake, Dk Ackson alijitoa, hatua
iliyoonekana ni kumpisha kada mwenye uzoefu zaidi, Job Ndugai.
Wakati
CCM wakisubiri uchaguzi wa mgombea wao, Rais John Magufuli alimteua Dk
Ackson kuwa mbunge na baadaye akachukua fomu za kuwania unaibu spika,
akiwa mgombea pekee wa chama hicho.
Tangu
aanze kuongoza Bunge, Dk Ackson amekuwa akikwaruzana na wabunge wa
upinzani, ambao walishawahi kuhusisha kuteuliwa kwake na Rais kuwa
mbunge ili apate mwanya wa kugombea unaibu spika, na mpango wa Serikali
kutaka kulidhibiti Bunge.
Akizungumzia
mkakati wao jana, Mbowe alisema kwa kuwa siasa haifanywi bungeni tu,
watakwenda kwa wananchi kuwashitaki viongozi wa Bunge.
Alisema
watafanya hivyo kwa kuwa kitendo cha kuwafungia wabunge wa upinzani
kuwatetea wananchi ndani ya Bunge, kinaweza kufanywa pia nje ya chombo
hicho.
“Tutawaamsha
wananchi nje ya Bunge kwa kuwa ni fursa hivyo tunakutana na wabunge
wote waliotimuliwa na tutaungana wote bila kujali chama cha siasa kwa
kuwa tumekubaliana kusimamia ajenda ya nchi na si ya chama chochote,” alisema Mbowe.
LHRC yataka wabunge warudishwe
Wakati
wabunge saba wakianza kutumikia adhabu ya kufungiwa kuhudhuria vikao,
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelitaka Bunge kuwarejesha
ili kuendelea na majukumu yao.
Mkurugenzi mtendaji wa kituo hicho, Dk Helen Kijo Bisimba
alisema hoja ya kuwafukuza wabunge hao kwa sababu ya kudai haki ya
kurushwa bunge ‘live’ ni kuwapokonya haki Watanzania waliowachagua
kwenda kuwawakilisha bungeni.
“Wabunge
hao wamechaguliwa na wananchi na wanatetea bunge hilo kurushwa ‘live’
kwa maslahi ya wananchi waliowatuma, halafu kiti cha Spika kinaamua
kuwafukuza bungeni.
"Endapo
ningepewa nafasi ya kuwashauri wapiga kura, ningewaambia kwenda
kushiriki vikao vya Bunge wenyewe kwa sababu wabunge wao wameondolewa
bungeni, hata mimi mbunge wangu wa Kawe ameondolewa,”alisema.
|
June 1, 2016
MBOWE:TUPO TAYARI KUTIMULIWA WOTE BUNGENI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment