RAIS
wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema hakuna nchi au jumuiya za
kimataifa zitakazomwondoa madarakani yeye kwa sababu amechaguliwa
kihalali na wananchi kwa kura nyingi kwa mujibu wa Katiba.
Dk
Shein alisema hayo wakati akizungumza na wanachama na wafuasi wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) katika matawi ya Wesha Tibirinzi, Pembeni Shengejuu
na Maziwa Ng’ombe, Micheweni katika ziara ya kuwafariji kutokana na
matukio ya hujuma zilizofanywa na wapinzani huko Pemba.
Aliwataka
wafuasi wa CCM na wanachama wake waliopo Pemba, wasibabaishwe na kauli
zinazotolewa na viongozi wa vyama vya siasa wanaopita na kudai kwamba
uchaguzi mwingine unakuja.
“Mimi
ndiye Rais halali wa Zanzibar nimechaguliwa katika uchaguzi ulioitishwa
na Tume ya Uchaguzi... wananchi msisikilize uvumi na kauli za wapinzani
zenye lengo la kuwababaisha na kuwayumbisha katika shughuli zenu za
maendeleo,” alieleza Dk Shein.
Dk Shein alisema amesikitishwa na kauli za uchochezi zinazotolewa na viongozi wa vyama vya siasa zenye malengo ya kuishawishi jamii kutengana na kugombana na kususiana hata katika shughuli za jamii ikiwemo misiba.
Alisema
kiongozi anayefanya vitendo vyenye lengo la kuwagawa wananchi kwa
malengo ya kisiasa huyo ameishiwa na hana nafasi katika jamii.
“Huyo kiongozi anayewashawishi wananchi kususia shughuli za jamii na maendeleo basi huyo ameishiwa kisiasa na hana nafasi katika jamii ya wananchi na ninyi mpuuzeni.Alikuwa na nafasi ya kushiriki katika uchaguzi lakini alisusa,” alieleza. Alisema viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) wameishiwa hoja kwa sasa na hawana la kufanya baada ya kugomea kushiriki katika uchaguzi halali wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu ambao umetoa nafasi kwa CCM kushinda katika uchaguzi wa kishindo.
Mapema
Dk Shein ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM aliwataka wanachama wa
chama hicho kutembea kifua mbele na kuachana na unyonge kwa sababu chama
chao ndiyo kilichoshika dola na kuunda serikali.
Akizungumzia yanayotokea Pemba, Dk Shein alisema, “Nimesikitishwa
na taarifa za matukio mbalimbali yanayofanyika huku Pemba ikiwemo watu
kususiwa maiti, kushushwa katika gari za abiria baada ya kuwa na itikadi
tofauti......haya matukio hayakubaliki na yanakwenda kinyume cha
maamrisho ya dini zote.”
Aliwataka
viongozi waliopewa majukumu kwa mujibu wa Katiba kufanya kazi zao na
kupambana na vitendo vya ubaguzi ikiwemo vya kuonewa kiholela wananchi.
|
June 1, 2016
SHEIN:HAKUNA MTU WALA NCHI YAKUWEZA KUNIONDOA MADARAKANI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment