WABUNGE
wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambao wamekuwa wakiingia bungeni
kusaini posho na kuondoka, wako hatarini kufutiwa posho kama wataendelea
kususa vikao vya Bunge kama walivyotangaza.
Hali
hiyo inatokana na hoja zaidi ya mbili zilizowasilishwa kwa Spika wa
Bunge kwa njia ya Mwongozo huku moja ikiwasilishwa na Waziri mwenye
dhamana ya Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe, zikikusudia kutaka
Bunge kufuta posho za wabunge hao.
Akizungumza
jana bungeni baada ya kuruhusiwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, Dk
Mwakyembe akitumia ibara za Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977
na Kanuni za Kudumu za Bunge, alitaka uongozi wa Bunge kutazama upya
kama wabunge hao wanastahili kulipwa posho.
Dk
Mwakyembe, kwanza alitumia Ibara ya 26 ibara ndogo ya kwanza na ibara
ndogo ya pili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo
aliinukuu; “Kila mtu ana wajibu wa kufuata na kutii Katiba hii na
sheria za Jamhuri ya Muungano. Kila mtu ana haki, kwa kufuata utaratibu
uliowekwa na sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya
Katiba na sheria za nchi.”
Baada ya hapo alinukuu tena Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 23, ibara ndogo ya kwanza na ya pili;
“Kila mtu, bila ya kuwapo ubaguzi wa aina yoyote, anayo haki ya kupata
ujira unaolingana na kazi yake, na watu wote wanaofanya kazi kulingana
na uwezo wao watapata malipo kulingana na kiasi na sifa za kazi
wanayoifanya. Kila mtu anayefanya kazi anastahili kupata malipo ya
haki.”
Kwa
kuzingatia ibara hizo za Katiba, alisema kwa kutumia nafasi yake ya
raia wa Tanzania na Waziri mwenye dhamana ya Katiba na Sheria, alihoji
kama haki inatendeka, kulipa posho na stahiki wabunge ambao hawakuingia
bungeni wala hawakuwa katika shughuli inayotambuliwa na Bunge, sawa na
waliokuwa wakifanya kazi bungeni.
Alitaka
Bunge lifafanue kwa kuzingatia ibara hizo za katiba kama ni haki kulipa
wabunge hao wa Ukawa, wanaoingia bungeni na kusaini ili walipwe posho,
kwa kubonyeza vitufe vya kielektroniki na kuingia bungeni kwa sekunde
chache na kutoka kwenda kupumzika.
Kuhusu wabunge waliosimamishwa kazi na Bunge, Dk Mwakyembe alihoji kama Bunge linazingatia Kanuni ya 75, ama la.
Kanuni hiyo inasema: “Mbunge
aliyesimamishwa kazi atatoka katika Bunge na hataingia tena katika
sehemu yoyote ya Ukumbi wa Bunge na maeneo ya Bunge kwa muda wote
atakapokuwa amesimamishwa, na atalipwa nusu mshahara na nusu posho
zinazoambatana na mshahara huo.”
Kabla
ya Mwongozo wa Dk Mwakyembe, juzi usiku Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali
Keissy (CCM) aliomba Mwongozo na aliporuhusiwa alimtaka Naibu Spika
aeleze kama kitendo cha wabunge hao wa Upinzani kuingia na kukaa muda
mfupi na kutoka bungeni, kinatofautiana na tatizo la wafanyakazi hewa
ambao wanapigwa vita na serikali.
“Kweli Mheshimiwa Naibu Spika, serikali inawaona na wewe unawaona, hii si kuiibia serikali? Au na sisi tuanze?” Alihoji Keissy.
Mbali
na Keissy, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM) aliomba
Mwongozo jana na kumtaka Naibu Spika kuzingatia Mwongozo wa Dk Mwakyembe
na Keissy, akieleza kuwa kama si dharau kwa Bunge, kumsimamisha mtu
kazi, halafu anaruhusiwa kuitisha mikutano ya kibunge jimboni.
Alimtaka
Naibu Spika ambaye ni mwalimu wa sheria, akubali iletwe hoja ya
kurekebisha Kanuni za Bunge ili adhabu inayotolewa kwa mbunge, imdhibiti
asifanye shughuli zozote ikiwemo mikutano ya hadhara wakati wa adhabu.
Akipokea
miongozo hiyo, Naibu Spika aliahidi kutolea uamuzi baadaye baada ya
kufanya mashauriano huku suala la adhabu likirejeshwa kwa Kamati ya
Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Wabunge
wa Ukawa kuanzia mwanzoni mwa wiki hii waliazimia kususa kuingia
bungeni katika vipindi vyote vitakavyoongozwa na Naibu Spika, kwa madai
kuwa anawaongoza kibabe kama wanafunzi na kuwa hajui uchungu wa kampeni
katika majimbo.
Hata
hivyo, juzi Dk Tulia aliwataka Watanzania wasikubali kupotoshwa na
Kambi Rasmi ya Upinzani, iliyoamua kususa vikao anavyoviongoza, kwa kuwa
kama wanaona amekosea, kuna fursa ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wake.
Kwa
upande wao, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imewasilisha kwa Ofisi ya
Spika wa Bunge kusudio la kumwondoa madarakani Naibu Spika wanayemtuhumu
kwa mambo sita ikiwemo upendeleo, ubabe na kufanya kazi kwa maslahi ya
Serikali, badala ya umma.
Kusudio
hilo la maandishi lilipelekwa katika ofisi hiyo jana na kupokelewa na
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah kwa niaba ya Spika, Job Ndugai
ambaye hakuwepo ofisini wakati huo.
Mbunge
wa Simanjiro, James ole Millya (Chadema) ndiye aliyewasilisha kusudio
hilo kwa niaba ya kambi hiyo ya upinzani na kuzungumza na wanahabari
kuhusu hatua hiyo, katika mkutano na vyombo vya habari.
|
June 3, 2016
MWAKYEMBE ATAKA MISHAHARA NA POSHO ZA WABUNGE WA UKAWA ZIFUTWE
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment