Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Prof. Justin Ntalikwa (mbele) akiongoza kikao cha uzinduzi wa Bodi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) uliofanyika jijini Dar es Salaam. |
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya madini Prof James Mdoe, akielezea historia ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) katika uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam. |
Baadhi ya wajumbe wa Bodi Mpya ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) wakifuatilia kwa makini hotuba ya uzinduzi wa bodi hiyo iliyokuwa inatolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Prof. Justin Ntalikwa.(hayupo pichani). |
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Prof. Justin Ntalikwa (mbele kulia) akimkabidhi vitendea kazi mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dk. Lightness Mzava, (mbele kushoto) mara baada ya uzinduzi wa bodi hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam |
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati
na Madini Prof. Justin Ntalikwa ( wa tatu kutoka kushoto waliokaa
mbele) Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini
anayeshughulikia masuala ya madini Prof James Mdoe ( wa pili kutoka
kushoto waliokaa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa
Bodi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) mara baada ya kumalizika
kwa uzinduzi huo.
……………………………………………………………………………
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati
na Madini Prof. Justin Ntalikwa amezindua bodi ya wakurugenzi ya
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na kuitaka bodi hiyo kuhakikisha
kuwa shirika hilo linaendeshwa kibiashara na kuchangia katika ukuaji wa
sekta ya madini.
Bodi hiyo iliyoteuliwa hivi
karibuni na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo
inaundwa na wajumbe watano ambao ni pamoja na Abdalah Musa, Dkt.
Coretha Komba, Felix Maagi, Dkt. Lightness Mnzava, John Seka chini ya
Mwenyekiti wake Balozi Alexander Muganda.
Profesa Ntalikwa alisema kuwa
STAMICO ni Taasisi ya Serikali iliyopewa jukumu la kushiriki katika
uwekezaji kwenye sekta ya madini kwa niaba ya serikali hivyo bodi ina
wajibu mkubwa wa kusimamia shirika kwa manufaa ya taifa kwa
kuhakikisha kuwa miradi yote iliyo chini ya shirika hilo inaendelezwa na
kusimamiwa ipasavyo ili kuipatia Serikali manufaa mbalimbali ikiwepo
gawio katika migodi ya ubia.
Aliendelea kusema kuwa kwa sasa
STAMICO inaiwakilisha serikali katika miradi mbalimbali ikiwa ni
pamoja na Mgodi wa Tanzanite unaomilikiwa kwa ubia kati ya Tanzanite
One Mining Limited asilimia 50 na STAMICO asilimia 50; Mgodi wa
Dhahabu wa Buckreef unaomilikiwa kwa ubia wa STAMICO kwa asilimia 45 na
TANZAM2000 kwa asilimia 55.
Alitaja miradi mingine kuwa ni
pamoja Mgodi wa STAMIGOLD wa Biharamilo unaomilikiwa kwa asilimia 100 na
kampuni tanzu ya STAMIGOLD; Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira kwa
asilimia 100 na Mradi wa Dhahabu wa Buhemba kwa asilimia 100.
Miradi mingine ni ya ununuzi wa
madini ya bati (tin) kupitia kampuni tanzu ya Kyerwa Tin Company
Limited na miradi ya utafutaji wa madini kwenye leseni mbalimbali za
utafutaji wa madini zipatazo 49 zinazomilikiwa na shirika.
Aliongeza kuwa shirika linatoa
huduma za uchorongaji na ushauri kwenye masuala ya madini pamoja na
kusaidia wachimbaji wadogo hasa kwenye masuala ya kiufundi.
Alisisitiza kuwa kutokana na
miradi mikubwa ya STAMICO, bodi ina kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa
miradi yote ya shirika hilo inaendelezwa kwa faida
“Katika kusimamia shirika,
mtazamo unatakiwa uwe ni wa kujiendesha siku za usoni kutokana na
kuendesha miradi yenye faida na kuleta gawio serikalini. Alisema Prof.
Ntalikwa
Aliendelea kusema kuwa ni vyema
shirika liendeshwe kwa mtizamo wa kibiashara ili liweze kushindana na
wadau wengine wanaowekeza katika sekta ya madini na kuleta manufaa
yenye tija kwa taifa.
Aliwataka wajumbe wa bodi hiyo
kupitia sera, sheria na miongozo mbalimbali katika sekta ya madini ili
waweze kuisimamia STAMICO kwa ufanisi pamoja na kuhakikisha kuwa
mikataba mbalimbali ambayo shirika linaingia inakuwa ni yenye
manufaa.
Alisisitiza kuwa pale
inapowezekana bodi inatakiwa kuboresha mikataba iliyopo kwa kukaa na
wabia ili pande zote ziweze kunufaika na manufaa yatokanayo na miradi
husika.
Wakati huohuo akizungumza katika
uzinduzi huo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini
anayeshughulikia masuala ya madini Prof James Mdoe alisema kuwa
STAMICO ina historia ndefu tangu kuanzishwa kwake miaka ya 1970
ambapo lilielekea kufa lakini lilirudi kwenye hadhi yake mwaka 2013
Alisema kuwa shirika la STAMICO
likisimamiwa ipasavyo, linaweza kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa
uchumi wa nchi kupitia sekta ya madini.
“ Shirika hili lina miradi mingi
na madini yapo mengi ambapo ninaamini kuwa iwapo itasimamiwa
ipasavyo shirika lina mchango mkubwa sana wa kuifanya sekta ya
madini kuchangia kwa asilimia kubwa katika pato la taifa,” alisema
Prof. Mdoe.
Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo
Balozi Alexander Muganda, akizungumza mara baada ya uzinduzi huo,
alisema kuwa anamshukuru Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter
Muhongo kuwa na imani na bodi hiyo na kuahidi kufanya kazi kwa bidii
katika kuhakikisha kuwa shirika hilo linapiga hatua kubwa katika
mchango wake kwenye pato la taifa.
Alisema kuwa bodi yake imejipanga
kuhakikisha kuwa shirika linasimamiwa kwa ufanisi mkubwa ili STAMICO
iweze kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi.
|
No comments:
Post a Comment