KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

June 1, 2016

SERIKALI IMEJIPANGA KUKARABATI UWANJA WA NDEGE WA MTWARA.

images
Na Fatma Salum- MAELEZO,
 Dodoma.
Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imetenga shilingi bilioni 10 katika mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Mtwara.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Edwin Ngonyani leo Bungeni Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtwara Vijijini Mhe. Hawa Ghasia lililohoji kuhusu ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Mtwara.
Mhe. Ngonyani alisema kuwa Serikali imeendelea kufanya matengenezo ya mara kwa mara katika uwanja huo na TAA inafanya tathmini ya uchakavu wa matabaka ya lami (Pavement Evaluation) ya njia ya kuruka na kutua ndege ili kubaini ukarabati stahiki unaotakiwa na matumizi ya fedha zinazohitajika na kazi hiyo ya tathmini inatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2016.
Aidha, Mhe. Ngonyani alieleza kuwa katika mpango wa muda mrefu, Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege inaandaa Mpango Kabambe (Master Plan & Concept Design) kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa uwanja huo kutoka daraja 3C la sasa kwenda daraja la 4E ili kuweza kuhudumia ndege kubwa zaidi hivyo kuwa kitovu cha usafiri wa anga kwa Ukanda wa Kusini.
“Ukarabati na upanuzi wa uwanja utahusisha miundombinu yote ya kiwanja ikiwemo taa na mitambo ya kuongozea ndege pamoja na majengo. Kazi hiyo ya uandaaji wa Mpango Kabambe na Usanifu wa Awali inatarajiwa kukamilika Julai 2016.” Alisema Ngonyani.
Ikiwa ni mpango wa muda mfupi, Mhe. Ngonyani aliongeza kuwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imeingia makubaliano na Kampuni ya British Gas (BG) kwa ajili ya kutumia taa zake ambazo ni za kuhamisha kwa ajili ya kuongozea ndege pale ambapo ndege itatakiwa kutua usiku katika uwanja huo.

No comments:

Post a Comment