Imeelezwa kuwa Barabara ya Namtumbo-Tunduru yenye urefu wa km 193 inatarajiwa kukamilika septemba mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati akikagua
maendeleo yaliyofikiwa katika mradi wa ujenzi huo ulioanza mwaka 2014.
Amesema kuwa ujenzi wa barabara ya
Namtumbo-Tunduru ambao umegawanyika katika sehemu tatu ambazo ni
Namtumbo-Kilimasera yenye urefu wa Km 60.7, Kilimasera-Matemanga yenye
urefu wa Km 68.2 na Matemanga-Tunduru yenye urefu wa Km 58.7 ujenzi wake
uko katika hatua nzuri.
“Nimekagua zaidi ya kilomita 300
na nimeridhishwa na hatua iliyofikiwa katika miradi hii, nawaomba
muendelee kuzingatia viwango vilivyowekwa na Serikali itaendelea kuwapa
miradi mingine”, amesema Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa
Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) mkoa wa Ruvuma Eng. Lazeck
Alinanuswe amesema kuwa sehemu ya ujenzi wa barabara ya
Namtumbo-Kilimasera Km 60.7 mkandarasi wa barabara hiyo amekamilisha kwa
asilimia 90 na baadhi ya sehemu zingine ujenzi unaendelea.
“Ujenzi wa barabara unaendelea
vizuri hadi sasa zimebaki asilimia kumi ili ukamilike kwa asilimia mia
moja na kuanza kutumiwa na wananchi”, amesisitiza Eng. Alinanuswe.
Ujenzi wa Barabara ya Namtumbo
hadi Tunduru yenye urefu wa Km 193 inajengwa kwa fedha za Serikali ya
Tanzania kushirikiana na Shirika la maendeleo la Japan (JICA), na Benki
ya maendeleo ya Africa (AfDB).
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
|
July 18, 2016
BARABARA YA NAMTUMBO-TUNDURU KUKAMILIKA SEPTEMBA.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment