KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

July 18, 2016

WAFANYAKAZI WA VODACOM WAPANDA MLIMA KILIMANJARO


Wafanyakazi  36 kutoka makampuni mbalimbali nchini  Afrika ya Kusini  ikiwemo kampuni ya mawasiliano ya Vodacom wameshiriki mpango wa kupanda mlima Kilimanjaro  kuchangia jamii ujulikanao kama TREK4MANDELA na fedha zitakazopatikana zitasaidia kuwapatia watoto wa kike elimu ya afya ya uzazi na taulo za kinga wakati wa hedhi kupitia taasisi ya Imbumba Foundation ambayo inaendesha mradi wa wasichana ujulikanao kama Caring4Girls nchini humo.
Mpango huu wa TREK4MANDELA umekuwa ukienda sambamba na makampuni ya Afrika ya Kusini kushiriki katika shughuli za  kijamii kila mwaka kama sehemu ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa muasisi wa Taifa la Afrika ya Kusini,Hayati Nelson Mandela na kwa mara ya pili kampuni ya Vodacom Tanzania imedhamini msafara wa wapanda mlima hao kwa kuwapatia mawasiliano.
Akiongea wakati wa kuwakabidhi vifaa vya mawasiliano,Mkuu wa Vodacom kanda ya Kaskazini, Henry Tsamburakis alisema kampuni ya Vodacom Tanzania imetoa vifaa vya mawasiliano ili kuwezesha msafara wa wapanda mlima hao hawapati tatizo la mawasiliano  na marafiki,ndugu na familia zao ikiwemo  kutuma picha za matukio wawapo katika safari hiyo ya kupanda  mlimani.
"Vodacom Tanzania tunajivunia kuweza kuwadhamini watalii na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni yetu kutoka Afrika ya kusini kwa mwaka wa pili mfululizo kwa kudhamini Mfuko wa Mandela ambapo kila mwaka watalii hawa huja nchini mwetu mwezi wa saba  kupanda mlima wa Kilimanjaro wakiwa na lengo la kuchangisha pesa kwa ajili ya  kusaidia watoto wa kike" alisema Tzamburakis.
 Alisema Vodacom imetoa vifaa maalumu vya mawasiliano (Routers) sita  zikiwa zimeunganishwa katika mtandao wa kasi  wa 4G huku zikiwa zimewekewa vifurushi vya GB 10 watakazoweza kutumia kwa muda wote watakapokuwa katika zoezi la kupanda mlima Kilimanajaro .
Akiongea kwa niaba ya wenzake kwenye msafara huo,Gerry Elsdon ameshukuru Vodacom kwa kuwafadhili mawasiliano ambayo yatarahisisha safari yao ya kupanda Mlima hadi kileleni “Kwa niaba ya wenzangu tunashukuru Vodacom Tanzani kwa kutupatia mawasiliano ya kuendelea kutuunganisha na wenzetu popote pale walipo”.Alisema Elsdon.
Kwa upande wake mratibu wa safari hiyo ,Richard Mabaso ambaye ni mwanzilishi wa taasisi ya Caring4Girls   alisema lengo la safari hiyo ni kuendelea kuchangisha fedha kwa ajili ya kununua Taulo za kike kwa watoto wa kike wasio na uwezo ili kuwasaidia kujihifadhi na kuendelea na  shughuli zao za kila siku kama kawaida wakiwa salama na wakijiamini.
"Tunatambua changamoto zinazowakabili watoto wa kike hasa wale walioko mashuleni pindi wanapoingia katika siku zao,kupitia Mfuko wa Mandela tumeendelea kuchangisha pesa kwa ajili ya kuwasaidia angalau kupata taulo ili waweze kuendelea na masomo bila ya kuwa na kikwazo." alisema Mabaso.
Jitihada za kupambana na changamoto za vipindi vya hedhi pia zimekuwa zikifanywa na taasisi mbalimbali hapa nchini mojawapo ikiwa Vodacom Tanzania Foundation ambayo imekuwa ikifadhili mradi wa Girl Power unaoendeshwa na Shirika lisilo la kiserikali la T-MARC ambao umewezesha kupunguza utoro kwa wasichana waliokuwa wanakosa  masomo kutokana na kukosa  vifaa vya kuwakinga wakati wa hedhi na kutokuwepo na miundombinu rafiki mashuleni.

No comments:

Post a Comment