PRETTY
binti mdogo mwenye umri wa kama mwaka mmoja na nusu unapomzungumzisha,
kama watoto wengine wenye afya na uhakika wa malezi anatabasamu na
kucheka.
Binti
huyu mdogo ambaye analelewa na familia iliyomuasili kwa malezi
(hajaasiliwa kisheria) ni miongoni mwa watoto kadhaa nchini ambao
wanafaidika na mpango mpya wa kusaidia watoto waliokumbwa na ukatili na
unyanyasaji.
Pretty
(ambaye si jina lake la ukweli-nimempa jina hilo kulinda haki yake)
maisha yake mpaka sasa ni kama kitendawili kibaya ambacho ni Mungu tu
alitaka kukifumbua.
Nasema
ni Mungu tu kwa kuwa Pretty aliokolewa kutoka katika shimo la choo
alilotumbukizwa akiwa ndani ya mfuko wa rambo uliofungwa vyema.
Sajini
taji (Staff Sergeant) Pundensiana Baitu wa Dawati la jinsia wilaya ya
Kipolisi Mbalizi, anasema kwamba Pretty wakati alipoopolewa katika choo
cha mtu binafsi alikuwa na hali mbaya sana kiafya na juhudi kubwa sana
ilifanywa na hospitali ya Meta kumrejeshea afya yake.
Akisimulia
tukio hilo la kuhudhunisha alisema kwamba usiku wa Machi Mosi, mwaka
jana alipokea simu iliyomtafadhalisha msaada ili kuokoa maisha ya mtoto
aliyetupwa katika choo kinachotumika, katika eneo la Mlimareli huko
Mbalizi.
|
Sajini
taji Pundensiana Baitu wa Dawati la jinsia wilaya ya Kipolisi Mbalizi
akizungumza na mwandishi wahabari wa Modewjiblog (hayupo pichani) hivi
karibuni.
(Imeandaliwa na Zainul Mzige wa Modewjiblog)
Alisema
wakati anajaribu kuwasiliana na askari kwenda kuona kama wanahitaji
msaada wa Kikosi cha zimamoto, akapokea simu nyingine kwamba wananchi
wamebomoa choo hicho na kumtoa mtoto huyo ambaye alikuwa amefungwa
katika mfuko wa rambo na kwamba alishaanza kuliwa na wadudu wa chooni.
Aidha
aliambiwa katika simu kwamba mtoto huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa
wiki moja alikuwa bado anapumua hali iliyomfanya aelekeze polisi
kuitengeneza PF 3 haraka na kumpeleka mtoto huyo katika hospitali ya
Ifisu ambao nao kutokana na kukosa vifaa vya watoto wa aina yake katika
hali ile, walimkimbiza hospitali ya Meta.
Anasema
yeye alifika asubuhi kuona hali ya mtoto huyo akiambatana na Ofisa
Ustawi wa Jamii na hakupendezwa na hali aliyomkuta nayo mtoto.
Anasema
kwamba juhudi za upelelezi kujua mama wa mtoto huyo hazikufanikiwa
kwani mtoto alitupwa katika choo binafsi karibu na klabu ya pombe. Hata
hivyo anasema baada ya kushindwa waliwaambia wananchi wa eneo hilo
kumtazama mtu ambaye wanamtilia shaka na kumfikisha kwao kwa mahojiano.
Mpaka wakati wa kuandika makala haya mtu huyo hajapatikana.
Anasema
kutokana na mfumo mpya wa familia ya mfano baada ya wao kama polisi
kukamilisha kazi ya usalama na kumkabidhi mtoto huyo kwa Ofisa Ustawi wa
Jamii, ofisa huyo alimtafuta mtu ambaye yuko tayari kulea mtoto na
kumkakabidhi kwao.
Sajini
taji huyo anasema kuwa kuna ongezeko la vitendo vya unyanyasaji na
ukatili dhidi ya watoto na kwamba jamii inatakiwa kubadilika na kukubali
wajibu wake katika kuhakikisha usalama wa mtoto.
|
Afisa
Ustawi wa Jamii Hospitali ya Kanda ya Nyanda za juu Kusini, Gerald
Mwaulesi akielezea tukio la mtoto Pretty mbele ya kamera ya Modewjiblog
jijini Mbeya hivi karibuni.
Anasema
kabla ya kuanzishwa kwa wilaya mpya wakati bado iko Mbeya amekuwa
akishuhudia vurugu nyingi kuhusu ukatili kwa watoto na kwamba dawati
lake inachofanya ni kutoa ushauri hasa kwa wadada ambao wanatoa mimba na
wengine kutupa watoto wanapopatikana.
Alisema
ingawa kuna taratibu ndefu za sheria, mfumo mpya uliokubaliwa na
serikali wa kupata familia ya mfano ni mfumo bora wenye kuhakikisha
malezi mema na kizazi bora kijacho.
Pretty
ambaye kwa sasa anaishi na familia ya mfano yenye watoto sita na yeye
akiwa wa saba katika kijiji cha Muvwa kilichopo kata ya Mshewe wilayani
Mbalizi ana uhakika na malezi kutokana na mfumo huo mpya.
Na
Si ajabu akikua hakuna mtu hata yeye mwenyewe atakayejua kwamba
aliokolewa kutoka kwenye shimo la choo alikotupwa na mama katili wiki
moja baada ya kuzaliwa kwake na kusaidiwa malezi yake na mfumo wa
familia ya mfano.
|
Dk Sipora Harison Kisanga wa UNICEF kanda ya Iringa akifafanua jambo kwa mwandishi wa habari wa Modewjiblog (hayupo pichani)
Dk
Sipora Harison Kisanga ambaye anafanyakazi na UNICEF kanda ya Iringa
anasema kwamba ulinzi na usalama wa mtoto ni eda ya wananchi wote kwa
ujumla, lakini kutokana na dosari zilizopo ndio maana UNICEF na Tanzania
zimetia saini makubaliano yanayowezesha maandalizi ya watu wa kuwapokea
watoto waliotelekezwa na wale wenye mazingira magumu ili nao waweze
kuwa sehemu ya familia zilizobora.
Anasema
kuufanya mfumo huo uwe na utekelezaji uliobora waliendesha mafunzo na
kutambua watu wanaoweza kukaa na mtoto, na baada ya kuwakagua wapo
katika orodha wakisubiri mtoto yeyote atakayepatikana.
Anasema
kutokana na maandalizi hayo ndio maana hata walipompata mtoto Pretty
walijua kwamba watampelaka Muvwa kwa familia ambayo iko tayari kupokea
mtoto wa aina yoyote na wa umri wowote.
Anasema
ni lengo la UNICEF kuhakikisha kwamba haki za watoto zinatekelezwa
ikiwamo ya ulinzi na usalama dhidi ya vitu na watu wabaya, huduma za
afya, huduma za elimu, haki ya kucheza na haki ya kufundishwa yaliyo
mema kutoka kwa wakubwa wao.
|
Afisa
Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Mbeya, Lilian Kilongumtwa akielezea
tukio la mtoto Pretty aliyetupwa kwenye shimo la choo jijini Mbeya kwa
mwandishi wa habari wa mtandao wa Modewjiblog.
Anasema
Ofisa huyo wa UNICEF kwamba Mradi wa familia ya mfano ulianzia Temeke
na sasa upo Mbeya, Mbarali, na Mbalizi kwa lengo lile lile kuwawezesha
watoto hawa kuwa na familia na kuwa salama kuliko kuwapeleka katika
vituo vya kulelea yatima.
Mama
anayemtunza mtoto huyo pamoja na mumewe, Mama Christer Eliston Mwashusa
anasema amefurahi sana kupata mtoto huyo kwani alikuwa tayari kumsaidia
kutokana na hofu ya Mungu aliyonayo.
Anasema
yeye angelifurahi kama mtoto angemuasili kisheria kwani hali ya sasa ya
ulezi pekee anaiona kama haimpi nafasi ya kufanyakazi yake vyema ya
kumtunza. Anataka awe mali yake moja kwa moja.
Anasema
amepata changamoto nyingi tangu alipomkuta mtoto Pretty hospitali ya
Meta, changamoto ambazo zilimuumiza kwanza kama mzazi kwa kutambua
kwamba mtoto yule hana wazazi na pia kwa kutambua kwamba ametelekezwa
kikatili.
|
Familia
Bw. Juma Mbuza (48) na Bi. Christer Mwashusha (43) inayomlea mtoto
Pretty wakifurahi jambo na binti yao baada ya mahojiano na mwandishi wa
habari wa Modewjiblog (hayupo pichani).
Pia
changamoto ambayo alikumbana nayo ni kule kutambua kwamba mtoto yule
kwa sababu ya kuwekwa chooni alikuwa na dhiki kubwa ya afya na hivyo
kumfanya kuwa dhaifu.
Anasema
hata wakati alipoanza kumtunza changamoto za afya yake zilikuwa kubwa
na hasa alipoambiwa kwamba ana ugonjwa ambao ameurithi kwa mama yake,
ugonjwa ambao ni upungufu wa kinga na kuanza kumlisha dawa za kufubaza
virusi vya UKIMWI kuanzia alipokuwa na miezi miwili hadi minne.
Hata
hivyo katika mahojiano na Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka hospitali ya
kanda ya rufaa Mbeya (Meta) aliyempokea mtoto huyo Gerald Godfrey
Mwambesi alisema kwamba Pretty hakuwa na virusi tangu awali walipompima
na kusema kwamba hata vipimo vya hospitali nyingine vilivyosema kwamba
ana virusi havikuwa sahihi.
Anasema
Pretty alipoteza nguvu ya kinga ya mwili kutokana na kukaa chooni kwa
muda na hivyo siku zilivyozidi ndivyo alivyokuwa akiongeza kinga.
Anasema
baada ya siku tatu ya kukabiliana na vidonda vyake vilivyotokana na
kutafunwa na wadudu chooni na baada ya wiki tatu alionekana kuwa nafuu
sana na ingawa mlezi alipata changamoto kiukweli mtoto huyo hakuwa na
virusi zaidi ya kupoteza kinga za kawaida ambazo zilitakiwa kurudishwa
taratibu.
|
Dada na kaka wa kufikia mtoto Pretty wakifurahi na mdogo wao mara baada ya kutoka shule.
Anasema
mtaalamu huyo kwamba waliongea na wataalamu wa watoto kuhusiana na
shida hiyo ya hospitali Mbalizi kumuona mtoto na virusi wakati wao
walimpima mara mbili bila kuviona na kusema kwamba hali hiyo inatokana
na maambukizi yaliyosababishwa na kutupwa ndani ya choo ambayo
yalihitaji tiba ya muda mrefu.
Mlezi
anasema kwamba baada ya miezi miwili ya kukaa na mtoto huyo kwa uzuri
aliona afya yake inadorora kiasi cha kuhitaji msaada wa tiba na kuanza
kwenda hospitali kupata msaada.
Anasema
hospitali aliyoenda ilisema mtoto ana maambukizi kutoka kwa mama na
kushauri tiba hivyo alipelekwa katika kiliniki ya Beira ambako walimpima
na kumwanzishia dozi waliyokuja kuikatisha baada ya kumpima tena
kutokana na ufuatiliaji wa hospitali ya Meta na kugundua kwamba hana
tatizo la maambukizi ya UKIMWI.
Mlezi
wa mtoto huyo alishukuru sana watendaji wa taasisi ya Kihumbe ambao
walimsaidia fedha za nauli kwenda katika hospitali kutetea afya ya
Pretty na kwamba baada ya matumizi ya dawa na dawa lishe mtoto huyo
mwezi uliopita (Juni 16,2016) aliambiwa kwamba mtoto wake hana
maambukizi tena.
KIHUMBE,
ni taasisi inayofundisha wawezeshaji namna ya kuwasaidia watoto
wanaoishi katika mazingira magumu hasa familia zao ili waweze kujimudu
wenyewe na kuondokana na matatizo hayo.
Baba
mlezi katika familia hiyo yenye watu saba akiwamo Pretty, Juma Mbuza
amesifu juhudi za mke wake katika kuhakikisha kwamba Pretty anapata
mapenzi yote ya kimama na kuendelea kustawi akiwa katika familia hiyo.
Anasema
familia yake inawiwa.kulea mtoto huyo kwa kuwa ndiyo ilikuwa nia yao
tangu awali na kwamba awali walitaka kuwachukua watoto waliotelekezwa
katika kijiji jirani kwenye tarafa yao.
|
No comments:
Post a Comment