HATIMA
ya nani atakuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ipo mikonini
mwa mwenyekiti mtarajiwa Rais Dk. John Magufuli, ambaye sasa yupo mbioni
kukabidhiwa mikoba ya chama hicho.
Nafasi
hiyo kwa sasa inashikiliwa na Katibu Mkuu anayemaliza muda wake,
Abdulrahman Kinana, ambaye ameshika nafasi hiyo tangu Novemba, 2012.
Jana
Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka, alisema hadi sasa maandalizi
yanakwenda vizuri na tayari wajumbe wataanza kuwasili mjini Dodoma
mapema wiki hii, kwa ajili ya Mkutano Mkuu utakaofanyika Julai 23, mwaka
huu.
“Suala
la nani ni Katibu Mkuu litaamuliwa na mwenyekiti mpya Dk. John
Magufuli, baada ya kukabidhiwa chama na Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Tunataraji wajumbe 2,465 watahudhuria na hata wakipungua basi ni
kidogo,” alisema
Msemaji
huyo wa CCM alisema kuwa baada ya Julai 23, kutakuwa na kikao cha
Halmashauri Kuu ambacho ndicho kitaamua juu ya mapendekezo ya mwenyekiti
mpya kama anabadili sekretarieti au laa.
“Kwa
sasa Katibu Mkuu bado ni Kinana hivyo sasa hapo ndipo kuna kitandawili
ambacho kitateguliwa na mwenyewe Rais Magufuli kama ataendelea na
aliyepo sasa au atakuja na mtu mwingine,” alisema Sendeka.
Alipoulizwa
kuhusu kuibuka kwa kundi la watu wanaompinga Rais Magufuli, asipigiwe
kura kwa ajili ya kukabidhiwa chama, alisema hakuna kitu kama hicho
zaidi ya taarifa hizo kuenezwa kwenye mitandao ya kijamii.
“Suala
la kuwepo kwa watu kumpinga Rais Magufuli asikabidhiwe chama si geni,
ingawa hadi sasa hatujaweza kumfahamu mwanachama yeote anayeendesha
mpango huu.
“Mambo
haya nahisi kuna kikundi cha watu kinajifurahisha katika mitandao ya
kijamii hivi inawezakana vipi wajumbe walewale waliomchagua Magufuli awe
mgombea wa CCM eti leo hii wageuke na kumpinga?
“…
hili si kweli na si geni kama unakumbuka hata mwaka 2002 wakati mzee
Benjamin Mkapa anawania uenyekiti kwa mara ya pili mambo kama haya
yalijitokeza na wale waliokuwa wanatajwa walikanusha na haohao ndiyo
wakawa mstari wa mbele kuhakikisha wanatafuta kura za kutosha,” alisema Sendeka.
Hata
hivyo hadi sasa bado Kinana amekuwa akipewa nafasi ya kuendelea kuwa
katibu mkuu ingawa mwenyewe amekuwa akitajwa na watu wake karibu kuwa
anahitaji kupumzika.
Polisi wachimba mkwara
Akizungumza
kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa,
Mrakibu Mwandamizi wa jeshi hilo mkoani hapa Mayala Towo, alisema
polisi wamejipanga kuufanya Mkoa wa Dodoma kuwa kisima cha amani wakati
wote na baada ya Mkutano Mkuu wa CCM.
“Amani
itakuwepo wana Dodoma na Watanzania wasiwe na wasiwasi ukija na nia
mbaya tutakachokufanya utawasimulia wenzako kwani kwetu amani ni wajibu
wetu,” alisema Mayala.
Alitoa
angalizo kwa wale watakaopokea na kuwaweka wageni katika nyumba zao
ambao lengo lao ni kufanya fujo kuwa jeshi hilo litawachukulia hatua
kali za kisheria.
“Usiwe
sehemu ya tatizo, kama unampokea mtu na kumweka kwako ili aje afanye
vurugu wa kwanza kuchukuliwa hatua utakuwa wewe mwenye nyumba,” alisema.
|
July 18, 2016
HATIMA YA ABDULRAHMAN KINANA MIKONONI MWA RAIS MAGUFULI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment