JESHI
la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini kwa kushirikiana na
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA)
imesitisha leseni za madereva 18 kutokana na mgomo walioufanya kupinga
wenzao kupelekwa mahakamani.
Wamiliki
wa mabasi 12 ambayo madereva hao walikuwa wanaendesha kwenda sehemu
mbalimbali nchini, wamepewa siku saba kujieleza ni kwa nini wasifutiwe
leseni za kutolea huduma hizo pamoja na kutakiwa kusitisha ajira kwa
madereva hao.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kamanda wa Kikosi cha
Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, alisema Julai 23 mwaka huu mkoani
Kagera, madereva wa mabasi hayo walifanya mgomo kupinga kitendo cha
madereva wenzao kupelekwa mahakamani, kukosa dhamana na kulala rumande
kutokana na makosa mbalimbali ya usalama barabarani ikiwamo kuendesha
kwa mwendo kasi.
Kamanda
Mpinga alisema dereva yeyote atakayeendesha gari kwa kasi ya zaidi ya
kilometa 90 kwa saa atafikishwa mahakamani na sio kutozwa faini kama
awali ili kuhakikisha matukio ya ajali yanapungua nchini.
Alisema
kutokana na hali hiyo madereva wanaoendesha mabasi yanayoanza safari
zake kwenye Manispaa ya Bukoba, walisitisha huduma kwa kushinikiza
Mahakama iwaachie wenzao waliokamatwa kwa makosa ya mwendo kasi.
‘’Serikali
haitavumilia kuona madereva wasiofuata sheria za usalama barabarani na
sheria za kazi na ajira. Jeshi la Polisi ndio tunawapa madereva mafunzo,
tunasajili vituo vya mafunzo na kuwapa leseni. Hivyo tunasitisha leseni
zao kwa mujibu wa sheria kwa kukiuka kanuni za leseni,’’ alisema
Mpinga na kuongeza kuwa askari watakaoachia madereva na kampuni za
mabasi kutembea kwa zaidi ya kilometa 90 kwa saa watachukuliwa hatua za
kinidhamu.
Mkurugenzi
wa Sumatra, Gilliard Ngewe, aliyataja mabasi pamoja na madereva
waliositishiwa leseni kuwa ni Hussein Tegatega na Miraji Kondo wa
Kampuni ya RS Express wanaoendesha basi lenye namba za usajili T 425 DDT
aina ya Zongtong linalotoka Bukoba kwenda Dar es Salaam.
Said
Omary na Amos Danney wa basi la Kimotico lenye namba za usajili T 966
CDY aina ya Nissan linalotoka Bukoba kwenda Arusha na madereva wanne wa
mabasi ya Princess Muro yenye namba za usajili T 166 DCA na T 923 DCT
yanayosafiri kutoka Bukoba kwenda Dar es Salaam.
Madereva hao ni Ally Mshuza, Twalibu Ondossy, Costa Andrew na Witness Lema.
Madereva
wengine ni Musa Tindwa na Gerald Beti wa Kampuni ya Osaka Raha
wanaoendesha basi lenye namba za usajili T 968 CPC linalofanya safari
zake Bukoba kwenda Dar es Salaam na Paul Ngussa wa basi lenye namba za
usajili T 810 BDW aina ya Scania linalotoka Bukoba kwenda Musoma, mali
ya Kampuni ya Bunda Express
No comments:
Post a Comment