Mchungaji
wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Ubungo jijini Dar es Salaam, Anthony
Lusekelo maarufu ‘Mzee wa Upako’ amesema kitendo cha viongozi wa CCM
kulitaja zaidi jina la Edward Lowassa katika Mkutano Mkuu Maalumu wa
chama hicho ni ishara kuwa Waziri Mkuu huyo wa zamani ni tishio.
“Nani! Lowassa…. jina lake kutajwa sana katika vikao vya CCM. Hiyo inaashiria kuwa ni mtu tishio. Ndiyo ni tishio,” alisema Lusekelo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Lusekelo
ambaye hivi karibuni, Rais John Magufuli alishiriki ibada katika kanisa
lake, alimzungumzia Lowassa baada ya kuulizwa swali juu ya mtazamo wake
kuhusu Mkutano Maalumu wa CCM ambao jina la mgombea huyo wa urais
kupitia Chadema na Ukawa lilitajwa na makada wengi wa chama hicho
tawala.
Alisema
hilo lilidhihirika hata katika mchakato wa CCM kupata mgombea wake wa
urais, kutokana na Lowassa kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa.
Alisema
kitendo cha Waziri Mkuu huyo wa zamani kuzua mjadala katika Mkutano
Mkuu wa chama hicho tawala sambamba na wimbi la makada wanaohama vyama
vyao, si mambo yanayopaswa kuwa mjadala kwa sababu uchaguzi ulishapita.
Huku
akisema: “Sizungumzi haya kwa ajili ya kujipendekeza, sihitaji ukuu wa
wilaya,” Lusekelo aliwataka viongozi kukataa kuendeleza uhasama wa
kisiasa na chuki kwa maelezo kuwa mwaka huu uwe maalumu kuzika tofauti
hizo, kufanya kazi kulijenga Taifa na kuhubiri amani na umoja.
Katika
mkutano huo, Lusekelo alipongeza kuimarika kwa vyama vya upinzani
akaponda mvutano ulioibuka bungeni akisema kukosa uzoefu kwa Naibu
Spika, Dk Tulia Ackson kulichangia huku akiunga mkono kauli ya Rais
kuzuia shughuli za siasa na kubainisha jinsi Rasimu ya Katiba ya Tume ya
Jaji Joseph Warioba, ilivyopendekeza kupunguzwa kwa madaraka ya Rais.
Jumamosi
iliyopita, katika Mkutano Mkuu wa CCM mjini Dodoma, uliomalizika kwa
Rais Magufuli kuchaguliwa kuwa mwenyekiti, mzimu wa Lowassa ulitawala
kutokana na kila aliyepewa nafasi ya kuzungumza ama kumtaja kwa jina au
kwa mafumbo.
Mwenyekiti
wa CCM aliyemaliza muda wake, Jakaya Kikwete ndiye aliyeanza
kuzungumzia hali ya mchakato wa chama hicho kupata mgombea wake wa
urais, kuwa ulikuwa mgumu na majaribu makubwa na kwamba wazee walifanya kazi kunusuru hali hiyo.
Katika
mchakato huo, CCM ilikata jina la Lowassa katika hatua za awali, jambo
lililosababisha kiongozi huyo kuhama na kundi la wanaCCM na kujiunga na
Chadema ambayo ilimteua kuwa mgombea wake wa urais.
Hata
hivyo, katika mkutano wake wa jana, Lusekelo alisema katika mchakato wa
chama hicho tawala kupata mgombea wake wa urais kulikuwa na watu wenye
majina makubwa, akiwamo Lowassa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje,
Bernard Membe.
“Niliwaambia
CCM, Membe huwezi kumpuuza, Lowassa naye huwezi kumpuuza maana wanataka
madaraka na kwa vyovyote lazima mtapata mtikisiko. Nikawaomba
waahirishe suala la kupata Katiba Mpya maana wasingelimaliza na muda
ulikuwa mfupi,” alisema na kuongeza: “Kama mwaka huu hautatumika kutibu majeraha yaliyotokea huko nyuma, tutaharibikiwa sana.”
Alisema
mchakato wowote wa uchaguzi na kura ya maoni ndani ya vyama huacha
mpasuko na watu hutumia dini na ukabila kubaguana, hivyo lazima baada ya
uchaguzi mambo hayo yamalizwe.
“Tunapaswa
kukumbuka kuwa wote ni Watanzania tusahau uchaguzi. Sasa ni wakati wa
kuijenga nchi. Amani inatengenezwa, na Mungu huwapa hekima maana kujenga
ni kazi na kubomoa ni rahisi, huu ni mwaka wa uponyaji na kurejesha
Taifa pamoja,” alisema Lusekelo.
Alisema
kuanza kubagua watu kwa sababu walitoka CCM kwenda Chadema au kutoka
Chadema kwenda chama tawala si jambo sahihi huku akitolea mfano mataifa
yaliyovurugika kwa kuendekeza siasa za chuki na uhasama.
No comments:
Post a Comment