KATIKA
kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kutaka serikali kuhamia
Dodoma, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba amesema
watendaji wa wizara hiyo wataanza kuhamia Dodoma kuanzia wiki ijayo.
Katika
hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa
Justin Ntalikwa amewataka wakuu wa idara na vitengo wote wa wizara hiyo
kuanza maandalizi ya kuhamia Dodoma na kuwa wametekeleza agizo hilo
ifikapo mwezi Septemba, mwaka huu.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana, Dk Tizeba alisema tayari watendaji wa wizara
hiyo wanaotakiwa kuhamia Dodoma wameanza kufanya maandalizi ya safari.
Alitoa
dokezo hilo mara baada ya kutoa taarifa kuhusu Mkutano wa
Ushirikishwaji wa Wadau kwenye Sekta ya Uvuvi, unaoishirikisha pia
Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi ya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar na wadau mbalimbali.
“Ni kweli hata sisi Wizara tuko kwenye maandalizi wiki hii, kwa sababu wiki ijayo tutahamia Dodoma, tunatekeleza agizo la Rais,” alisema Waziri Tizeba.
Kauli
ya Waziri Tizeba imekuja siku moja baada ya Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa kutangaza kuhamia Dodoma ifikapo Septemba mwaka huu, huku
akiwataka Mawaziri na Naibu Mawaziri kumfuata.
Waziri
Mkuu alisema ameshaagiza ukarabati kwenye nyumba yake ukamilishwe ili
ifikapo Septemba aweze kuhamia na kuwataka mawaziri kufanya hivyo kwa
sababu kila Waziri ana nyumba na ofisi ndogo mjini Dodoma.
Nayo
Wizara ya Nishati na Madini imetoa waraka ikiwataka wakuu wa idara na
vitengo wote wa wizara hiyo kuanza maandalizi ya kuhamia Dodoma ifikapo
mwezi Septemba mwaka huu.
Agizo
hilo lipo katika waraka uliotolewa na Kabibu Mkuu wa Wizara ya Nishati
na Madini, Profesa Justin Ntalikwa jana na nakala yake kutumwa pia kwa
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Katibu
Mkuu huyo alisema agizo hilo linatokana na kauli iliyotolewa na Rais
Magufuli katika Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
uliofanyika mjini Dodoma hivi karibuni, ambapo alisisitiza azma ya
serikali yake kuhamia Dodoma.
Alisema
pamoja na kauli ya Rais, watendaji hao wanatakiwa kuanza maandalizi ya
kuhamia Dodoma ifikapo Septemba kutokana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
kuahidi kuhamia Dodoma mwezi huo na kuwataka Mawaziri na Naibu Mawaziri
nao kumfuata.
No comments:
Post a Comment