JAJI
Mkuu, Mohamed Chande Othman amempongeza Rais John Magufuli kwa kutoa
zaidi ya Sh bilioni 12.3 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa majengo ya
mahakama nchini.
Ametoa
pongezi jana wakati akizindua Mahakama ya Wilaya ya Siha na Mahakama ya
Mwanzo Bomang’ombe, iliyopo wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro.
Kwa
mujibu wa Jaji Chande, ujenzi huo utaanza hivi karibuni kwa wilaya na
mikoa ambayo hazina huduma hiyo, ili kusogeza huduma za mahakama karibu
na wananchi, hali itakayosaidia kupunguza mrundikano wa kesi katika
mahakama nyingine.
Wilaya
26 na mikoa sita hapa nchini, zinakabiliwa na ukosefu wa huduma za
mahakama za wilaya pamoja na mahakama kuu, hali inayosababisha wananchi
kutumia gharama kubwa kutafuta huduma hiyo katika wilaya na mikoa
mingine.
Alieleza
kuwa fedha zilizotolewa na Rais Magufuli, zitakwenda kwenye ukarabati
na ujenzi wa mahakama za mwanzo, ili watendaji wa mahakama hizo wafanye
kazi katika mazingira bora, ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa mahakimu na
makarani wa kutosha.
Alisema
mbali na fedha hizo, pia anaishukuru serikali kwa kuongeza bajeti ya
idara ya mahakama kwa mwaka wa fedha 2016/2017, ambapo wanakusudia
kujenga mahakama za wilaya 10, Mwanzo 10, ambapo alitaja baadhi ya mikoa
ambayo haina Mahakama Kuu kuwa ni mkoa wa Singida, Lindi na Mara.
Alisema
asilimia 74 ya kesi za mashauri yapo katika mahakama za mwanzo, ambapo
mashauri zaidi ya 1,150 yanayosikilizwa katika mahakama hizo hapa
nchini, ambapo aliziagiza mahakama za mwanzo na wilaya kuhakikisha kesi
zote za mashauri zinafunguliwa katika mahakama hizo.
Aliagiza
ifikapo mwisho wa mwaka huu, hataki kuona wala kusikia kesi iliyomaliza
muda wa miezi sita bado inaendelea kupoteza muda na gharama bila ya
sababu za msingi, na kutoa wito kwa jeshi la polisi kujitaidi
kukamilisha upelelezi wa kesi ili kuwajengea wananchi imani na kutoa
fursa kwao kudai na kupata haki zao mahakamani kwa wakati.
Awali
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Moshi, Jaji Aishieli Sumari,
alisema changamoto inayoikabili idara ya mahakama ni pamoja na ukosefu
wa watumishi na mahakimu katika wilaya ya Siha, ambapo mahakama hiyo
tangu kufunguliwa kwake Aprili 4 mwaka huu, tayari imepokea mashauri 87
na yaliyosikilizwa ni 19 kutokana na wilaya kutokuwa na hakimu.
No comments:
Post a Comment