Serikali
ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kusitisha zoezi la
kubadili Vyuo vya Ufundi kuwa Vyuo Vikuu kwa nia ya kuinua vijana,
kukuza na kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Hayo yamesemwa jana
na Naibu Waziri wa Wizara ya Kazi, Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu
Wenye Ulemavu. Antony Mavunde alipoalikwa kama mgeni rasmi katika
mahafali ya kwanza ya vijana waishio katika mazingira magumu
yaliyofanyika katika Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA),
jijini Dar es Salaam.
Mhe. Mavunde alisema
kuwa Serikali imeshaanza kuchukua hatua za awali za kuimarisha elimu na
stadi mbalimbali za ufundi nchini ambapo moja ya hatua hizo ni
kusitisha utaratibu wa kuvibadili vyuo vya ufundi kuwa vyuo vikuu na
imefanya hivyo kwa sababu ya kutambua umuhimu na mahitaji makubwa ya
wataalamu wanaohitimu katika vyuo hivyo kwenye soko la ajira.
“Serikali
itaendelea kusimamia sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi ya mwaka
1994 ambapo pamoja na mambo mengine, sera hiyo inaweka msisitizo katika
kuweka mazingira na kutoa elimu ya ufundi stadi katika ngazi mbalimbali
ili kuendana na mahitaji ya mafundi sanifu nchini”, alisema Mhe. Mavunde.
Naibu Waziri huyo aliongeza
kuwa amefarijika sana kuona vijana wamepatiwa mafunzo ya elimu ya
ujasiriamali, stadi za maisha pamoja na kuunda vikundi vyao vya kuweka
na kukopa ambavyo ni muhimu sana kwa wakati huu ambao Tanzania ya
Viwanda inaandaliwa.
Pia alitoa
rai kwa wazazi wenye vijana walemavu kuhakikisha wanatoa ruhusa kwa
vijana hao kuungana na vijana wengine kushiriki katika fursa mbalimbali
zinazotokea ili nao waweze kujenga uchumi wa Taifa.
Aidha, Mhe. Mavunde aliiomba
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kujitolea kuwasaidia vijana hao kwa kuwapa
elimu juu ya Mifuko hiyo ili watambue umuhimu wa kuhifadhi fedha zao
ambazo zitakuja kuwasaidia uzeeni.
Elimu
ya vijana waishio katika mazingira magumu ni Mradi wa miaka mitatu
unaofadhiliwa na Umoja wa Jumuiya ya Nchi za Ulaya na kutekelezwa na
Shirika lisilokuwa la kiserikali la Plan International, mradi huo
unagharimu kiasi cha Euro 3,874,984.53 na unatekelezwa katika Mikoa ya
Dar es Salaam, Morogoro, Pwani, Lindi na Mtwara.
|
July 19, 2016
SERIKALI YAJIPANGA KUSITISHA KUBADILI VYUO VYA UFUNDI KUWA VYUO VIKUU
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment