BODI
ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) imeagiza
kusimamishwa kwa wakurugenzi sita, mameneja watano na mhandisi mmoja wa
shirika hilo kupisha uchunguzi, kubaini wahusika katika tuhuma za
ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na
taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi, manunuzi ya ardhi na
ajira.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Profesa Samwel Wangwe, alikiri jana
usiku kusimamishwa kwa vigogo hao 11, kupisha uchunguzi wa tuhuma
zilizoelekezwa kwao.
“Ni
taarifa sahihi hizo. Kulikuwa na tuhuma katika ripoti ya ukaguzi, kwa
hiyo tumeamua wakae pembeni ili kupisha uchunguzi, hawajafukuzwa kazi.
Taarifa hiyo ya kusimamishwa ni sawa sawa,” alisema Profesa Wangwe jana usiku.
Kwa
mujibu wa taarifa kwa wafanyakazi, iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi
Mkuu wa NSSF, iliwataja wakurugenzi sita waliosimamishwa kuwa ni Yacob
Kidula (Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi), Ludovick Mrosso
(Mkurugenzi wa Fedha) na Chiku Matessa (Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na
Utawala).
Wengine
ni Sadi Shemilwa (Mkurugenzi wa Udhibiti Hadhara na Majanga), Pauline
Mtunda (Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Mahesabu ya Ndani) na Crescentius
Magori (Mkurugenzi wa Uendeshaji).
Aidha,
taarifa hiyo iliwataja mameneja waliosimamishwa kuwa ni Amina Abdallah
(Meneja Utawala), Abdallah Mseli (Meneja wa Uwekezaji), Mhandisi John
Msemo (Meneja wa Miradi), Davis Kalanje (Mhasibu Mkuu), Wakili Chedrik
Komba (Meneja Kiongozi – Mkoa wa Temeke) na Mhandisi John Ndazi (Meneja
Mradi).
Taarifa
hiyo kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, ilisema kwamba uamuzi huo
umefanywa na Bodi chini ya Profesa Wangwe iliyokutana Julai 15, mwaka
huu kutokana na taarifa mbalimbali za wakaguzi wa hesabu na shughuli za
uendeshaji wa shirika hilo la umma.
“Bodi
ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii chini ya Uenyekiti
wa Profesa Samwel Wangwe katika kikao chake cha 106 kilichofanyika
tarehe 15 Julai, 2016 kimeagiza kusimamishwa kazi kwa wakurugenzi sita
(6), mameneja watano (5) na mhandisi mmoja ili kupisha uchunguzi kubaini
wahusika katika tuhuma za ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na
kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa
miradi na manunuzi ya umma na ajira,” ilieleza taarifa hiyo.
Hivi
karibuni, NSSF ilitajwa katika vyombo vya habari kuhusu tuhuma zikiwamo
za ununuzi wa ardhi usiofuata taratibu za manunuzi ya umma, kuwapo kwa
ubadhirifu na ajira za upendeleo katika shirika hilo, ukiwataja wahusika
kuwa ni baadhi ya wakurugenzi wa shirika hilo.
|
July 19, 2016
WAKURUGENZI 6 WA NSSF WASIMAMISHWA KAZI KUPISHA UCHUNGUZI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment