Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea na utaratibu wa kutoa
tahadhari kwa wananchi na maelekezo ya hatua za kuchukua katika
kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu. Huu ni mwendelezo wa
utoaji wa taarifa ya kila wiki, kuhusu mwenendo wa ugonjwa huu kama
tulivyoahidi. Hadi kufikia tarehe 18 Julai 2016, jumla ya wagonjwa
22,306 wametolewa taarifa, na kati yao, watu wapatao 345 wamepoteza
maisha, tangu ugonjwa huu uliporipotiwa mnamo mwezi Agosti 2015
Takwimu zinaonyesha kuwa, katika
wiki hii inayoishia tarehe 18 Julai 2016, idadi ya wagonjwa wa
Kipindupindu walioripotiwa ni 54 na hakuna aliyepoteza maisha. Wagonjwa
wote waliotolewa taarifa walitoka mkoa wa Morogoro (Morogoro mjini 31,
Ulanga 20) na Arusha (Arusha mjini 3). Ikilinganishwa na wiki iliyopita
idadi ya wagonjwa imeongezeka ambapo kulikuwa na idadi ya wagonjwa 38
bila kifo.
Ninawapongeza uongozi na
watumishi wa afya wa Mikoa ya Arusha na Morogoro, kwa kuendelea kutoa
taarifa za ugonjwa wa Kipindupindu. Aidha ninatoa rai kwa Mikoa mingine
wahakikishe usahihi wa taarifa wanazotoa na kujiridhisha hakuna kweli
wagonjwa wa Kipindupindu katika Mikoa yao. Ningependa kusisitiza kwamba
Wizara yangu haitasita kuwachukulia hatua Waganga Wakuu wa Mikoa
watakaobainika kutotoa taarifa zisizo sahihi za wagonjwa wa Kipindupindu
na magonjwa mengine ya mlipuko.
Hatua tuliyoifikia katika
kupambana na mlipuko huu inatutaka tuendelee kuzidisha juhudi za
kupambana na ugonjwa huu kwa kusimamia kikamilifu maelekezo na miongozo
stahili inayotolewa na Wizara yangu ili kuutokomeza kabisa ugonjwa huu.
Hivyo ni muhimu Mikoa yote kuendelea kuchukua hatua za tahadhari ili
kuzuia maambukizi na pia kuendelea kutoa taarifa sahihi kila siku na
kusimamia kikamilifu hatua mbalimbali za udhibiti wa mlipuko huu.
Tunaendelea kuisihi jamii
kuungana na Halmashauri, Mikoa pamoja na Wizara katika juhudi za
kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu kwa kuzingatia
yafuatayo:
Wizara inapenda pia kuwajulisha
kuwepo kwa taarifa ya wagonjwa 4 wa ugonjwa wa kupooza kutoka katika
Mikoa ya Dodoma na Tabora katika Halmashauri za; Kongwa (2), Kaliua (1)
na Urambo (1). Wagonjwa hawa waliopata ugonjwa wa kupooza wa ghafla
waligundulika kuwa na ugonjwa wa polio baada ya sampuli zilizochukuliwa
na kupelekwa maabara kwa ajili ya upimaji, ikiwa ni zoezi la kawaida la
ufuatiliaji wa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo, kuthibitisha kuwa na
virusi vinavyosababisha polio.
Itakumbukwa kuwa nchi yetu
ilitangazwa rasmi kuwa mojawapo ya nchi za Afrika zisizokuwa na ugonjwa
wa polio tarehe 26 Novemba, 2015, na taarifa hii imechukuliwa kwa uzito
na Wizara yangu. Wizara imekwisha kuchukua hatua za haraka za kudhibiti
ugonjwa huo ambapo Timu ya Wataalam ilitumwa kwenda Mkoani Dodoma na
Tabora na mikoa ya jirani ili kufanya ufuatiliaji wa kina na kutoa
ushauri wa kuzuia kusambaa kwa virusi vya polio. Hadi sasa hakuna
wagonjwa wapya walioripotiwa na hakuna ongezeko la wagonjwa katika
Halmashauri ambazo zimegundulika kuwa na wagonjwa
Uwepo wa wagonjwa hao wanne wenye
polio ni kielelezo cha umuhimu wa kuendelea kufuatilia kwa ukaribu
magonjwa yote yanayozuilika kwa chanjo. Hivyo Wizara yangu inapenda
kutoa rai kwa wadau wote na taasisi zinazofanya kazi katika jamii na
vyombo mbalimbali kuendele kuhamasisha jamii ili watoto wote wapate
chanjo kulingana na ratiba. Aidha, waongeze juhudi katika kutoa taarifa
kwenye vituo vya huduma za afya vilivyopo karibu mara wanapoona au
kupata taarifa ya mtoto yoyote anayepata ulemavu wa ghafla pasipo sababu
yoyote.
Wizara inaendelea kuwapongeza na
kuwashukuru wadau wote kwa jitihada za dhati zinazoendelea kutekelezwa
katika kusimamia kikamilifu miongozo inayotolewa na Wizara ili
kutokomeza magonjwa ya milipuko, ikiwa ni pamoja na wataalamu wa sekta
mbalimbali, Mashirika ya Kimataifa, Watumishi, Mikoa na Halmashauri
pamoja na waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla.
|
July 19, 2016
TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI, PAMOJA NA MLIPUKO WA UGONJWA WA POLIO LILILOTOLEWA NA WAZIRI WA AFYA MHE.UMMY MWALIMU
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment