Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekuwa ikitekeleza afua mbalimbali za
mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU nchini ambazo zimepelekea kupungua
kwa viwango vya maambukizi ya VVU kitaifa kutoka wastani wa asilimia 7
mwaka 2007-2008 hadi kufikia asilimia 5.1 mwaka 2011-2012. Mafanikio
haya yamefikiwa kutokana na ushirikiano wa karibu kati ya Wizara na
wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na wale wa utekelezaji wa moja kwa
moja wanaofanya kazi na mikoa yote Tanzania bara. Aidha kumekuwa na
uitikiaji mzuri kutoka kwa wananchi katika utekelezaji wa afua hizo.
Sambamba na mafanikio haya,
tafiti mbalimbali hapa nchini zimethibitisha kuwepo kwa kiwango cha juu
cha maambukizi ya VVU miongoni mwa makundi maalum yaliyo katika hatari
zaidi ya maambukizi kuliko kiwango kilichopo miongoni mwa jamii ya
kawaida. Makundi haya ni pamoja na Wanawake wanaofanya biashara ya ngono
ambayo maambukizi ya VVU ni asilimia 26, Watu wanaojidunga sindano za
madawa ya kulevya (asilimia 36) na Wanaume wanaoshiriki ngono baina yao
(asilimia 25). Aidha, makundi haya yamekuwa na muingiliano wa karibu
sana na wana jamii ya kawaida, na hivyo kupelekea hatari ya kutofanya
vizuri katika udhibiti wa maambukizi ya VVU nchini.
Hali hii ilisababisha kuwepo na
umuhimu wa kuongeza nguvu katika afua mbalimbali za kukabiliana na
ongezeko la maambukizi ya VVU miongoni mwa makundi haya, pamoja na jamii
ya kawaida ili kudhibiti VVU. Kwa mantiki hiyo, Wizara kwa kushirikiana
na wadau mbali mbali walikubaliana mikakati mahsusi ya kutoa huduma
bora na rafiki kwa watu wa makundi maalum kwa kuzingatia sheria,
taratibu, mila na desturi za taifa letu.
Pamoja na nia njema na jitihada
za pamoja baina ya Wizara na wadau katika mapambano dhidi ya UKIMWI,
imebainika kwamba baadhi ya wadau wanaotekeleza shughuli za makundi
maalum wamekuwa wakikiuka taratibu za kiutendaji hasa suala la
kuihusisha Wizara na Mikoa husika wanakofanyia kazi kuhusu uanzishwaji
na/au utekelezaji wa baadhi ya shughuli wanazozifanya. Aidha pia katika
baadhi ya maeneo, wadau hao wamekuwa wakitekeleza shughuli ambazo ziko
kinyume na makubaliano waliyoingia na Wizara ya Afya.
Miongoni mwa shughuli
zinazokinzana na mila na desturi zetu ni pamoja na usambazaji wa
vilainishi. Ni kweli kuwa Wizara imezuia usambazaji wa vilainishi na
tayari tumewasiliana na wadau hao ambao wameahidi yafuatayo:
Wizara inawapongeza na
kuwashukuru wadau wote kwa jitihada za dhati zinazoendelea kutekelezwa
na katika kusimamia kikamilifu miongozo inayotolewa na Wizara yenye
lengo la udhibiti wa ugonjwa wa UKIMWI.
Imetolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
19 Julai 2016
|
July 19, 2016
TAMKO LA WIZARA KUHUSU MATUMIZI NA USAMBAZAJI WA VILAINISHI KWA AJILI YA UDHIBITI WA MAAMBUKIZI YA UKIMWI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment